Pages

Sunday, April 28, 2013

UNAMSHANGAA WENGER NA WACHEZAJI WA JEROJERO, VIPI KUHUSU DORTMUND?



Wenger
ARSENE Wenger anasajili wachezaji wa jero jero. Ukimwona Wenger anatoa buku basi ujue chenji inarudi. Maneno haya ya kejeli yanatawala kwenye vibanda vya kuonyesha mechi za soka mitaani.
Vitu kama hivi, ndivyo vinavyotia raha kutazama mpira katika vibanda vya mtaani. Kuna maneno yanayovutia sana kwenye sehemu hizi; Mikel Arteta huku anaitwa 'pitch manager', Ramires anaitwa 'mzaramo', Luis Nani 'msomali', Lionel Messi huku anaitwa 'kijini', wengine wanamwita 'kijiji'.
Kuna majina mengi huku, Shaun Wright-Phillips wanamwita 'kazi bure',

Rio Ferdinand wanamwita 'teja', mashabiki wa Manchester United wao wanamwita 'baba mwenye nyumba', Ryan Giggs anaitwa 'babu', Thierry Henry 'chogo' na Robin van Persie wanamwita 'hakunaga.'
Majina kama hayo na misemo mingi kama 'kulima kwenye zege', 'tiatia maji', 'kupaki lori', 'kukusanya kijiji' na mengine mengi ndio yanayotia raha kutazama mechi za soka kwenye vibanda vya mitaani.

Mashabiki wengi huku ni wafuasi wa Ligi Kuu England. Wamegawana timu za kuzishabikia. Upinzani mkubwa huku, ni wa Arsenal na Man United. Hili limetawala sana, kwani hata kama watakuwa kwenye vibanda hivyo kutazama mechi baina ya Manchester City dhidi ya Chelsea, bado stori zitabaki kuwa juu ya Arsenal na Man United.

Hili halikwepeki, kwasababu inaaminika ndizo timu zenye mashabiki wengi hapa nchini ukilinganisha na timu nyingine kama za Man City, Chelsea, Liverpool na Tottenham Hotspur. Hata wanaoshabikia timu za Barcelona, Real Madrid au Bayern Munich, wengi wao bado ni mashabiki wa timu hizo mbili, Arsenal au Man United.

Ukata wa mataji unaowakabili Arsenal, ukiacha mashabiki wenyewe wa timu hiyo kumlalamikia kocha wao, Wenger kutofanya usajili wa haja, wapinzani wao mashabiki wa United wanawakejeli kwamba, wanasajili wachezaji wa jero jero, kwamba kocha wao ni bahili, anataka akitoa buku, basi chenji irudi.

Lakini, Wenger amebaki kuwa kwenye msimamo huo huo wa kusajili wachezaji wake wa bei chee na bado anaiwezesha timu hiyo kushiriki mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa zaidi ya misimu 14 mfululizo. Mfaransa huyo, hana kikosi chenye gharama kubwa, lakini bado hakijaweza kutoka nje ya 'top four' kwa zaidi ya misimu 10, licha ya kwamba suala la mataji limeota mbawa kwenye timu hiyo tangu 2005.

Haya tuliweke mezani suala hili la wachezaji wa jero jero, kwa maana ya wachezaji wa gharama nafuu. Je, kuna ulazima wa kuwa na mchezaji wa kumsajili wa gharama kubwa ili timu ifanye vizuri? Je, hiyo inaweza kuwa sababu ya timu kushindwa kufanya vizuri kwa kuwa na wachezaji wa bei chee?

Wiki hii ilikuwa na maajabu makubwa katika soka la Ulaya. Usiku wa Jumanne, ilikuwa siku ya Bayern Munich. Kutokana na ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Barcelona na usajili wa kumnasa Mario Gotze kutoka kwa mahasimu wao Borussia Dortmund, ilionekana kama ni mwanzo mgumu unaotarajia kutokea kwenye kikosi cha BVB siku za hapo baadaye.
Kloop akiwa na Gundogan

Usiku wa Jumatano mambo yalikuwa tofauti, lakini hali ilizidi kuwa ngumu kwa upande wa La Liga, wakati wawakilishi wao wengine kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, Real Madrid kukumbana na kipigo kizito Signal Iduna Park. Hapa ni wakati kikosi cha Jurgen Klopp, BVB kilipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya mabingwa hao wa Hispania, los Blancos.

Wanachokifanya Dortmund katika miaka ya hivi karibuni, hakionekani kuisha hamu. Wakitokea kwenye kufilisika kifedha si zaidi ya muongo mmoja uliopita, sasa ni kama wameweka mguu wao mmoja kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na hii yote ni faida ya matunda ya kazi yao.

Mabingwa hao wa Ujerumani wa msimu uliopita, hawana fedha na wala hawanolewi na kocha mwenye jina kubwa. Ni ukweli usiopingika kwamba, wakati Klopp anachaguliwa kuinoa timu hiyo, kulikuwa na wasiwasi kwamba kama kocha huyo angeweza kuisaidia timu hiyo kurudisha hadhi yake kwenye Bundesliga.
Lakini, anachokifanya tangu wakati huo kimeonekana dhahiri na kuifanya Dortmund kuwa kwenye hadhi kubwa kabisa kiuchezaji. Katika kila idara, BVB walikuwa imara zaidi ya Madrid.

Klabu iliyojipatia umaarufu na sera yao ya Galacticos, Real Madrid imekuwa na kawaida ya kununua wachezaji wote bora katika sayari hii.
Kuanzia Alfredo Di Stefano hadi Cristiano Ronaldo, kumepita wachezaji wengi sana mahiri waliowahi kuichezea klabu hiyo ya Santiago Bernabeu, huku wengine wakiendelea kuwapo kwenye timu hiyo hadi sasa.
Kikosi cha sasa cha Borussia Dortmund, kinaundwa na vijana wengi. Nuri Sahin, alikuwa mchezaji muhimu wakati wananyakua ubingwa wa Bundesliga mwaka 2011, akiwa kijana aliyetokea kwenye akademi ya klabu hiyo, aliyekwenda kwa mkopo kwenye ligi ya Eredivisie, kabla ya kuhamia jumla Madrid, aliweza kufanya makubwa BVB.

Msimu uliofuata, wakicheza bila ya staa huyo wa kimataifa wa Uturuki (Nuri Sahin), walifanikiwa kuwa na Shinji Kagawa na Robert Lewandowski, ambao iliwasajili kwa dau la pamoja la euro milioni 5.1, waliochukua mikoba na kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa huo wa Bundesliga, tena kwa kuweka rekodi ya kuwa na pointi nyingi zaidi.

Sawa, wakati BVB wakifurahia mafanikio hayo ya ndani, Madrid nao ilikuwa hivyo hivyo. Wakiongozwa na mchezaji ghali zaidi, waliyemsajili kwa euro milioni 94, Cristiano Ronaldo, ambaye alikuja kusaidiana na wachezaji wengine waliosajiliwa kwa gharama kubwa kama Karim Benzema, Fabio Coentrao, Sergio Ramos, Xabi Alonso na Angel Di Maria, los Blancos waliweza kuvunja utawala wa Barca katika soka la Hispania, kwa kunyakua ubingwa wa La Liga cha Real Madrid na Dortmund kumenyana, basi kungefanya mechi hiyo kuwa bora kabisa, lakini haikuweza kuwa hivyo. Dortmund waliwafanya vibaya wapinzani wao hao, ambapo Lewandowski, Ilkay Gundogan na Marco Reus walionyesha kiwango bora kabisa kilichomwacha hoi Jose Mourinho na timu yake.

Ulikuwa unyanyasaji mkubwa kwa Madrid, timu ambayo ilikuwa inafukuzia taji lake la 10 la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Luka Modric, usajili wao mkubwa waliofanya mwaka jana kwa ada ya euro milioni 30, alipotezwa kabisa ndani ya uwanja na Gundogan, ambaye aliigharimu BVB moja ya sita ya dau hilo la Modric.

Na mbaya zaidi, Mcroatia huyo alikuwa amekidhi vigezo vyao. Kuna mchezaji hapa, Kaka, nyota wa Mbrazil, ambaye msimu huu ameanzishwa mechi 10 pekee, lakini gharama yake ni kubwa kuliko kikosi kizima cha Dortmund kilichocheza usiku huo wa Jumatano.
Mats Hummels, Reus na Gotze kwa pamoja mshahara wao ndio anaochukua Cristiano Ronaldo. Kutokana na gharama za malipo ya kikosi hicho kuwa na uwiano mzuri, Madrid ni wazi kabisa watakuwa wanaionea wivu Dortmund.

Real Madrid wanaweza kuwa na thamani kubwa pengine mara mbili dhidi ya wapinzani wao wa Ujerumani (euro milioni 475 kwa 254), lakini hawana kile kitu ambacho Dortmund wanacho; ari, hamasa na umoja.
Hadithi ya Dortmund kwa sasa ni moja ya habari njema kusikilizwa na klabu yoyote yenye kuishi kwa matumaini. Klabu kama Arsenal itahitaji kutumia hadithi za Dortmund kama sehemu ya mfano uliohai wa kufanya kisichotarajiwa hata kama watakuwa na kikosi chenye thamani ndogo.

Dortmund wameweza kulionyesha hilo kwa kufanya vyema licha ya kucheza dhidi ya timu zenye utajiri mkubwa, kuanzia Manchester City na Malaga, ambazo zinatumia fedha za Waarabu na hata Shakhtar Donetsk.
Na kama wataweza kuwafunga Bayern katika mechi hiyo ya fainali, basi huu utakuwa ni msimu wa aina yake kwa upande wao, hasa ukizingatia The Bavarians wamenyakua ubingwa wa Bundesliga tayari na wanaonekana kushinda vita ya kuinasa saini ya Gotze, lakini ushindi wa taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, utawaweka kwenye vita kubwa.

Ubingwa huo wa Ulaya, kwa miaka ya hivi karibuni umekuwa ukinyakuliwa kwa nguvu ya fedha, kwa maana ya kuwa na vikosi vyenye gharama kubwa. Lakini, kwa sasa BVB wanaweza kuleta mapinduzi na kunyakua ubingwa huo na wachezaji wake wa jero jero.
Fedha zinaweza kusaidia kununua mchezaji staa, lakini haziwezi kusajili mpambanaji. Ukitazama kikosi cha Dortmund kilichoanza usiku wa Jumatano na thamani zao kwenye mabano, utaweza kuona ukweli halisi wa jambo hilo.

Weidenfeller (huru), Pisczek (huru), Subotic (€4.5m ), Hummels (€4.2m ), Schmelzer (huru ), Gundogan (€5.5 ), Bender (€1.5 ), Kuba (€3.05 ), Gotze (huru), Reus (€17.1m ) na Lewandowski (€4.75 ) na kufanya jumla ya euro milioni 40.6, ambazo hazifikii hata gharama aliyosajiliwa Ricardo Kaka peke yake kutoka AC Milan.

Kikosi cha Real Madrid kilichoanza katika mechi hiyo na gharama zao za usajili kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Lopez (€3.5m ), Ramos (€27m ), Pepe (€30m ), Varane (€10m ), Coentrao (€30m ), Khedira (€14m ), Alonso (€35.4m ), Ozil (€18m ), Modric (€30m ), Ronaldo (€94m ) na Higuain (€12m ) na jumla yake ni euro milioni 303.9.

No comments:

Post a Comment