Pages

Sunday, April 28, 2013

ARSENAL NA KISA CHA KUUZA HAMMER NA KUNUNUA BAJAJI


LONDON, England
NA sasa mashabiki wa Arsenal wamepanga kuchelewa kufika uwanjani hii leo wakati timu yao itakapomenyana na Manchester United, katika mchezo mgumu kabisa wa Ligi Kuu England, katika Uwanja wa Emirates.

Kinachowafanya kuwa hivyo ni kwamba hawataweza kuvumilia maumivu ya kuwashuhudia wachezaji wao wakijipanga mistari miwili na kisha kuwapigia makofi United wakati wa kuingia uwanjani, ikiwa kama ishara ya heshima kwa mabingwa hao wa ligi msimu huu.

Na kinachouma zaidi ni kwamba makofi hayo yatamhusu nyota wao wa zamani, Robin van Persie - ambaye aliihama timu hiyo mwaka jana na kutimkia Old Trafford, alikokwenda kufanya makubwa na timu hiyo kutwaa ubingwa.

Pengine kitendo hicho cha mashabiki kinaweza kisionekane kuwa cha kimichezo, hasa ukizingatia United iliwahi kuzifanyia timu nyingine siku za nyuma wakati ilipotinga uwanjani kucheza dhidi ya timu ambayo imetoka kutwaa ubingwa.
Lakini, hawana jinsi - wanaumizwa hivyo kama wataamua kufanya hivyo hawataonekana kuwa ni watu wa ajabu. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anaweza kuona kitu cha kawaida kwa kukubali kujipanga mstari na kuwapigia makofi United, ambao wamefanikiwa kuurejesha ubingwa huo uliokuwa umenyakuliwa na mahasimu wao, Manchester City msimu uliopita.

Na kitendo cha kumshuhudia kijana wao wa zamani, Robin van Persie akiingia kukanyaga unyasi wa Emirates akiwa na kikosi cha mabingwa, hilo pengine litakuwa shambulio kubwa sana dhidi yao, kwenye soka, kwenye maisha na funzo kwamba mtu unapata malipo kwa kile unachokifanya.

Hii pia inatoa funzo kwamba kama unataka kufanikiwa basi ubahili ukae kando. Kocha wa United, Sir Alex Ferguson, alilifanya hilo mwishoni mwa msimu uliopita, ambapo alikubali kutoa pauni milioni 22 kumpata Van Persie, kitu ambacho kimelipa msimu huu.

Kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na kile alichotumia Wenger katika kuwasajili washambuliaji wawili kuziba pengo hilo la Van Persie. Alitumia pauni milioni 13 kumsajili Olivier Giroud kutoka Montpellier na pauni milioni 11 kumnasa Lukas Podolski kutoka Cologne.

Wenger anaweza kubisha na kudai kwamba amepata wachezaji wawili katika dau ambalo angepata mchezaji mmoja, lakini jambo hilo unaweza kulifananisha na mtu anayejaribu kuuza gari lake la Hammer na kisha ananunua bajaji mbili au tatu na kuona kitu cha kawaida tu.
Sawa, Giroud amefunga mabao 17 katika kikosi hicho cha Arsenal katika mikikimikiki yote msimu huu na Podolski amefunga mara 14, lakini hawawezi kuwa Van Persie.

Wapangwe nyota hao wawili pamoja, hawawezi kuifanya timu kuwa tishio zaidi ya mchezaji huyo mmoja tu, Van Persie anapokuwa ndani ya kikosi. Arsenal bana, imeuza Hammer na kukunua bajaji mbili.
Na sasa bajaji zitaweza kufanya kazi ya kusomba abiria, lakini kama utalishindanisha kwenye mbio, basi Hummer itaibuka mshindi hapo na kutwaa medali zote kama jambo hilo litafanywa kuwa mashindano. Tayari kama Ligi Kuu England ingekuwa mbio, basi Van Persie ameshinda hapo dhidi ya Giroud na Podolski.

Alex Ferguson alitambua kabisa Van Persie ni mchezaji muhimu aliyekuwa akikosekana kwenye kikosi chake, hivyo alimhitaji kwa nguvu zote ili kuongeza kitu fulani katika timu yake, hasa baada ya kupokwa ubingwa mwaka jana na Man City. Hapo alifanya uamuzi wa akili kabisa.
Matokeo yake hapo, United imetwaa taji lake la 20, huku Van Persie akitikisa nyavu mara 24 katika mechi 34 ilizocheza timu hiyo hadi kufika sasa kwenye ligi hiyo.

Van Persie alisema kwamba ameihama Arsenal kwa sababu alitaka kutwaa mataji — na hilo ameweza kulifanya ndani ya miezi 12 tu ndani ya Old Trafford kwa kuweza kufanikiwa kile alichofeli kwa miaka nane aliyodumu na Washika Bunduki.

Kwa kufanya hivyo, ametuma ujumbe kwa Arsenal kwamba wanaweza kuwa bora na tishio kwa kusajili mchezaji mmoja tu wa pauni milioni 30, kuliko kununua wa mafungu kwa pauni milioni 15. Van Persie atakuwa ameisaidia sana Arsenal.

No comments:

Post a Comment