Pages

Thursday, April 25, 2013

SHOMARI KAPOMBE AUGUA, KUIKOSA MECHI YA LEO TAIFA DHIDI YA RUVU SHOOTING



SIMBA imepata pigo kubwa baada ya beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe kuugua malaria kabla ya mechi yao ya leo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kapombe anatazamiwa kuikosa mechi hiyo, ambayo ni muhimu kwa Simba kushinda ili iweza kuwa na matumaini ya kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza  jijini, Daktari wa timu hiyo, Cosmas Kapinga, alisema Kapombe anasumbuliwa na malaria hivyo hataweza kucheza katika mechi hiyo.

Kapinga alisema Kapombe amepewa mapumziko hadi atakapopata nafuu  ambapo jana aliondolewa katika kambi ya timu hiyo iliyoko Bamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.

Alisema kutokana na hali yake, anatarajia kupumzika ili awe fiti zaidi katika mechi yao dhidi ya Polisi Morogoro, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Liewig amekua na imani na kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo, kutokana na kikosi chake kimekamilika katika  idara zote.

Liewig alisema kukosekana kwa Kapombe si tatizo kubwa katika kikosi chake, kwani pengo lake linatarajiwa kuzibwa na beki mwingine.

 Alisema wachezaji ambao wamebaki wanaweza kufanya kazi nzuri na kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.

Simba tayari wametema ubingwa wa ligi hiyo, kutokana na kuwa hata  kama watashinda mechi zao nne zilizosalia hawataweza kuifikia Yanga inayoongoza kwa pointi 56.

Timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36, huku Azam FC ikiwa ya pili yenye pointi 47 na Kagera Sugar inashika nafasi ya tatu kutokana na pointi 40.


No comments:

Post a Comment