Pages

Thursday, April 4, 2013

RHINO FC: HAIKUWA KAZI RAHISI KUFUZU KUCHEZA LIGI KUU, TULIJIPANGA NA TULIPAMBANA PIA


Unaweza kusema ni umri wa mtoto aliyezaliwa hadi kuhitimu elimu ya msingi kwani ni takribani miaka 12 bila mkoa wa Tabora kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Mirambo kushuka mwaka 2001.
Ilikuwa timu iliyoleta changamoto kwenye ligi kuu zamani iliitwa daraja la kwanza na kuweza kuwakilisha Tanzania bara kwenye kombe la Muungano mwaka 1993 lakini baada ya kushuka mkoa wa Tabora ulisahaulika kabisa kwenye ramani ya soka na kufanya mashabiki wa mkoa huo kukosa burudani.
Kutokana na Mirambo kushuka ilibaki historia ya majina ya wachezaji waliowahi kuwika wakiwa na timu hiyo kama Quresh Ufunguo, Wastara Baribari, Jobe Ayoub, Dionis Paul, Said Swed “Scud”, Douglas Muhani, Daddy Phares na akina marehemu Said John, Abbas Mchemba na wengine wengi.
Leo sipo kukuletea historia ya Mirambo ila nimekukumbusha kidogo ili kukuleta karibu uvute kumbukumbu ya mkoa wa Tabora kisoka ulivyowahi kuwika.  Msimu wa 2013 utakaoanza Septemba kiu ya mashabiki imekatwa na Rhino Rangers, timu inayomilikiwa na Jeshi la Wanachi kambi ya Tabora (JWTZ).
Rhino Rangers ilisajiliwa mwaka 1987 na ilianza kushiriki ligi daraja la nne wilaya ya Tabora mjini na baadae Ligi ya mkoa wa Tabora kipindi hicho ilichukulia michezo kama burudani kwa wafanyakazi baada ya kazi za kutwa.
Mchezaji Victor Hagaya wa Rhino akiwa amebebwa na mashabiki baada ya timu yake kushinda mchezo dhidi ya Polisi Dodoma ambao ndio walifikisha pointi 29 ambazo zisingewezwa kufikiwa na timu yoyote na kufanya kuhesabu wameshafuzu kucheza ligi kuu.

Mwaka 2008 JWTZ kambi ya Tabora iliona kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa timu inapata mafanikio na kuona siku moja inashiriki ligi kuu ili kutoa burudani kwa wana Tabora pia ajira kwa vijana wenye uwezo wa kusakata kabumbu la uhakika.
Kuhakikisha lengo linafikiwa iliundwa kamati ya watu tisa wa kusimamia na kuhakikisha Rhino Rangers inafanya vizuri na inafika mbali.
Kamati hiyo ilikuwa inaundwa na
Meja Prosper Masawe- Mwenyekiti,
Captain Samwel Mwaila- Makamu Mwenyekiti,
Clarence Kambona- Katibu,
Grayson Kawele - Katibu Msaidizi, 
Haji Kubeja - Mweka Hazina
Osward Mlaponi, Issa Habibu, Gift Emanuel na Steven Luziga ni wajumbe.

Baada ya kamati kupatikana na kuanza kazi 2008 Rhino Rangers ilichukuwa Ubingwa wa wilaya ya Tabora Mjini na Mkoa wa Tabora pia kwenye mwaka huo na kufanikiwa kuwakilisha mkoa wa Tabora kwenye mashindano ya kanda yaliyofanyika Shinyanga.
 
Mashabiki wa Rhino wakifuatilia kwa makini mpambano wa timu yao kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora
Ikiwa kwenye kituo cha Shinyanga 2009 ilipata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu zilizokwenda kwenye kituo cha Dar es salaam 2010 ambacho kilikuwa kinaundwa na washindi toka kila kanda.

Ikiwa kwenye kituo cha Dar es Salaam Rhino Rangers ilifanikiwa kupanda daraja la kwanza na kwenda kwenye kituo cha tisa bora kilichofanyika Tanga 2011, kituo ambacho ili uweze kuwa mwenyeji lazima ulipe milioni 25 kwa shirikisho la soka nchini (TFF)
Wakiwa kwenye kituo cha Tanga, timu za JKT Oljoro, Moro United na Coastal Union zilipata nafasi ya kucheza ligi Kuu, Rhino Rangers ikishindwa kupata nafasi ikarudi kujipanga tena kwani ilibaki kwenye daraja la kwanza.

Mwaka 2012  tisa bora ilichezwa Morogoro, timu za Polisi Moro, JKT Mgambo ya Tanga na Tanzania Prison ya Mbeya ndizo zilizofanikiwa kupenya na kufanikiwa kuingia ligi Kuu.

Uongozi wa Rhino Rangers haukukata tamaa bali walichukulia kama changamoto na kurudi kujipanga na hapa wanasema ligi kuchezwa kwa kituo ndio ilikuwa inasababisha timu zenye uwezo kupokwa nafasi  kauli ambayo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (TAREFA) Yusuph Kitumbo.

“Mkoa ulikuwa unanunua kituo kwa milioni 25 ambazo zilikuwa zinalipwa kwenye ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF) na zilikuwa hazirudishi hivyo mkoa uliakikisha timu yake inapanda daraja hata kama uwezo wake ni mdogo, hivyo waliwatumia waamuzi” alisema Clarence Kambona.

Pia anasema ushahidi wa timu zilizopanda daraja wakati huo na kushuka msimu huo ni Moro United na msimu huu kuna Polisi Moro ambayo ipo kwenye hatihati ya kushuka na kushukuru ligi kuchezwa nyumbani na ugenini.

“Mfumo wa kituo ulikuwa wa ukandamizaji kwani timu zilikuwa zinabebwa pasipo kuwa na uwezo akatolea pia mfano kituo cha Kigoma kuwa na uzalendo kwani JKT Kanembwa ilibebwa lakini ilipokuja kucheza nyumbani na ugenini ikashindwa kuchomoza zaidi ya kushinda michezo ya nyumbani ikajikuta inafungwa michezo ya ugenini” alitabainisha Clarence Kambona ambaye ni Katibu wa Rhino Rangers.

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) baada ya kuona na kujiridhirisha kuwa mfumo wa ligi uliokuwepo haukidhi haja ilibadilisha mfumo wa ligi na kuondoa ligi za vituo na kurudisha madaraja na kuamua ligi zichezwe kwa mfumo wa nyumbani na ugenini lakini wakaweka mikoa kwenye kanda ili kupunguza ukali wa gharama kwani ligi haina mfadhili.

Rhino Rangers ambayo ilikuwa Kundi C linalohusisha timu za mikoa ya kanda za magharibi, ziwa kati na kaskazini ilifanikiwa kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu kuu baada ya kujikusanyia pointi 32 kwenye michezo  14 iliyocheza.

Pia Kambona anasema wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Rhino Rangers inafanya vizuri kwenye ligi Kuu ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya ufundi itakayoshirikisha uongozi wa chama cha Soka Tabora na uongozi wa serikali wa mkoa huo kwani umoja ndio utakaweza kusaidia timu kufanya vema.

“Tunatoa kipaumbele kwa wazawa wa Tabora kwani wametupa ushirikiano wa hali ya juu na hamasa ya soka Tabora imerejea na kwa kushirikia na wadau na serikali naamini tutaweza kuipeleka Rhino Rangers tunapotarajia”, alisema.

Kambona anasema kwa sasa kambi imevunjwa lakini baadae wataita wachezaji wote wenye uwezo waje wacheze ili kamati ya ufundi itakayotajwa baadae ipate kuchagua wale wenye uwezo na baadae kuwasajili ili kuunda Rhino Rangers bora kama zilivyo timu zingine za majeshi ambazo zinaleta changamoto kwenye ligi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA) Yusuph Kitumbo anasema kuwa wapenzi wa soka wa Tabora ili Rhino Rangers ipate mafanikio na waweze kuziona Simba na Yanga zinakuja kucheza kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi wanatakiwa waweke mbele Rhino Rangers kwanza na Tabora kwanza.

“Wanatakiwa waweke Rhino Rangers kwanza na Tabora kwanza mbele kwani kwa kipindi cha miaka 14 inametosha kujifunza hivyo ushirikiano wao ndio utasaidia timu ifanye vizuri siyo Simba na Yanga zinakuja halafu wanaanza kuzishangilia na kuicha Rhino Rangers” alisema Kitumbo

Kitumbo alisema Usimba na Uyanga wanatakiwa waweke kwenye mechi zingine ambazo Rhino Rangers haichez,  ikiwezekana ziwe zile za kimataifa.

Pia Kitumbo anasema uongozi wa Rhino Rangers unatakiwa uendelee kuwa karibu na wao kama walivyofanya na kwa sababu timu yao mashabiki wa Tabora wanaona kama mali yao kwani haina zile tabaka za kijeshi itakuwa rahisi kuendelea kufanya vizuri.

Uongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (TAREFA) umeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha unaipandisha Tabora kwenye medani ya soka kama ilivyowahi ikiwa ni pamoja na kuanzisha kozi za waamuzi, makocha na utawala ili kuhakikisha mchezo wa soka unaendeshwa na wataalamu.

Kwa kuwa Rhino Rangers itatumia uwanja wa Ally Hassan Mwinyi katika michezo yake ya nyumbani TAREFA imesema imewasiliana na wamiliki wa uwanja huo chama cha Mapinduzi ili kuufanyia ukarabati ikiwa ni pamoja na kuweka vyoo vya nje kwani hakuna vyoo zaidi ya vilivyopo kwenye vyumba vya wachezaji.





No comments:

Post a Comment