Pages

Thursday, April 25, 2013

DNA ZA BABU SEYA HAZIKUPELEKWA KWA MKEMIA MKUU


IKIWA ni miaka takriban tisa (9) tangu kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samweli Manyele  amebainisha kuwa Sampuli ya Vinasaba (DNA) za mwanamuziki nguli Nguza Vicking  “Babu Seya” na watoto wake hazikufikishwa ofisini kwake kwa ajili ya kupimwa.

Profesa Manyele, aliyasema hayo juzi mjini Arusha, wakati akijibu maswali ya washiriki wa warsha iliyolenga kutoa elimu kwa wafanyakazi wa idara za upelelezi, ustawi wa Jamii, Mahakama na Wanasheria wa Sekta binafsi iliyofanyika mjini hapa.

Katika warsha hiyo, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Seif Mangwangi alitaka kujua kama vipimo vya DNA vya Babu Seya, watoto wake na mtoto aliyelawitiwa viliyochukuliwa kama vilifanyiwa kazi na ofisi ya Mkemia Mkuu, ambapo Profesa Manyele alijibu kuwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali haikupokea Vinasaba vya watuhumiwa hao kwa ajili ya kuvipima.
“Sampuli za Vinasaba hazikuja kwetu, ziliishia kwenye vyombo vingine vya Serikali. Lakini pia si kila kesi inayosikilizwa lazima ihitaji vipimo vya DNA,” alisema Prof. Manyele.

Prof. Manyele alisema kwa upande wa kesi ya Babu Seya na watoto wake ilikuwa na mlolongo wa mambo mengi yaliyokuwa yakiangaliwa ya kihistoria, hivyo vipimo vya vinasaba vilichukuliwa lakini havikufanyiwa kazi kama ambavyo inadhaniwa.

“Hata kama tulihitaji DNA, sisi hatulazimishi Mahakama kutumia vipimo vyetu. Kama upande wao walijiridhisha na ushahidi hilo ni lao ama pia ushahidi ulijitosheleza,” aliongeza.
“Kesi nyingine zinamalizika kwa upelelezi wa kawaida wa polisi au hospitali na vipimo vya DNA si vya mwisho vinavyofanya uamuzi wa kesi uwe A au B,” alisema Prof. Manyele.

Juni 25 mwaka 2004, Babu Seya na wanaye walihukumiwa kifungo cha Maisha jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo, Addy Lyamuya aliwatia hatiani kwa makosa 23 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo.

Mara baada ya hukumu hiyo ambayo iliibua simanzi kubwa kwa ndugu, jamaa na wapenzi wa muziki hapa nchini, Babu Seya na wanaye walikata rufaa katika Mahakama Kuu ambapo Januari 27 mwaka 2005, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo aliitupilia mbali rufaa yao.
Katika rufaa yao, Babu Seya na wanae walikuwa wakipinga hukumu iliyowatia hatiani kwa makosa 10 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo makosa ambayo walidaiwa kuyatenda kati ya Aprili na Oktoba mwaka 2003, eneo la Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam.

Hata hivyo katika kupigania haki yao Wasanii hao, walikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Haya hivyo Alhamisi ya Februari 11, 2010, rufaa yao iligonga mwamba baada ya kuwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Mbangu (Mashine) na Francis Nguza (Chichi) na kuyatupilia mbali mashitaka 18 kati ya 23 yaliyokuwa yakiwakabili wanamuziki hao kwa maelezo kuwa hayatambuliki katika sheria za nchi. Mahakama ya Rufaa ilikazia hukumu ya Kifo cha maisha kwa Babu Seya na mwanaye mmoja Papii Kocha, ambao wanaendelea kutumikia kifungo hicho katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment