Pages

Sunday, April 7, 2013

CHELSEA YAIFUNGA SUNDERLAND 2-1 NA KUPAA HADI NAFASI YA TATU




Chelsea leo imepigana kufa na kupona na kuibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Sunderland.
Licha ya kuwa fikra za mashabiki wengi ziko katika pambano la wapinzani wa jiji la Manchester, United na City, litakalopigwa kesho, kulikuwa na burudani za kutosha katika siku ya leo katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Uingereza, ambapo jumla ya mechi tano zilipigwa.

Katika mechi ya awali, Liverpool waliokuwa nyumbani walijikuta wakishindwa kuonyesha makali yao pamoja na kutumia faida ya kuwa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na West ham United.

Mechi hiyo licha ya kutawaliwa na mashambulizi ya kutosha na burudani kubwa, bado ilishindwa kutoa mshindi baada ya washambuliaji wa pande zote mbili kushindwa kuzitumia kikamilifu fursa kadhaa ambazo wangeweza kuzitumia vyema na kuzipatia timu zao ushindi.

Katika mechi zilizopigwa baada ya pambano hilo, Tottenham waliokuwa nyumbani na ambao wako kwenye hati hati ya kuondolewa kwenye nafasi ya nne na wapinzani wao wa jadi Arsenal, walilianza pambano lao dhidi ya Everton kwa staili ya kufurahisha baada ya mshambuliaji Emanuel Adebayor, kuwafungia bao katika sekunde ya 39 tu toka kuanza pambano hilo.

Huku mashabiki wao wakiwapa sapoti ya hali ya juu, Spurs walishindwa kuwapa nguvu mashabiki wao baada ya dakika ya 15 kukubali Phil Jagielka kuwasawazishia wageni na mwanzoni mwa kipindi cha pili Kevin Mirallas, kuwaongezea Everton bao la pili.

Baada ya hapo, pambano hilo lilifunguka zaidi ambapo wenyeji walikuwa wakihaha kusaka bao la kusawazisha wasiadhirike nyumbani huku Everton wakitaka kupata pointi tatu muhimu ambazo zingewaweka kwenye nafasi nzuri ya kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao.

Juhudi za wageni zilielekea kuwanyong’onyeza mashabiki wa Spurs ambao huku wakijua kuwa wanaadhirika nyumbani, walijikuta wakilipuka kwa furaha baada ya Gylfi Sigurdsson, kuwasawazishia bao dakika za lala salama za mechi hiyo.

Kwa sare hiyo, Spurs wameshuka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 58 sawa na Chelsea ambao wamekwea hadi nafasi ya tatu kwa uwiano mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa, na wako mbele ya Arsenal kwa pointi mbili tu huku Arsenal wakiwa na mechi moja ya kiporo.

Kule darajani, kocha mpya wa Sunderland, ambaye maisha yake nje ya soka yamekuwa gumzo kuliko yale ya uwanjani toka asaini kuwanoa vijana hao, Paul De Canio, alionekana kuanza vyema kibarua cha kuinoa Sunderland baada ya kufanikiwa kuwabana vilivyo Chelsea waliokuwa nyumbani kiasi cha kusababisha mechi hiyo kwenda mapumziko wageni wakiwa wanaongoza kwa goli la kujifunga la Cesar Azpilicueta dakika ya 44.

Hata hivyo, huku mashabiki wa Chelsea wakianza kumrushia maneno ya kejeli kocha wao Rafael Benitez, kocha huyo mhispania alirejesha kikosi chake kipindi cha pili kikiwa katika mtazamo mpya ambapo juhudi zao zilifanikiwa kusafanya Sunderland nao kujifunga kunako dakika ya 46 kupitia kwa Matthew Kilgallon, kabla ya Branislav Ivanovic, kuwafungia bao la ushindi kunako dakika ya 54.

Kwa ushindi huo, Chelsea wamekwea hadi nafasi ya tatu na kuzishusha chini Tottenham na Arsenal, hali ambayo inazidi kuongeza utamu wa mchuano wa kuwania nafasi za kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Katika mechi nyingine pia iliyopigwa jioni hii, Newcastle walifanikiwa kujipatia pointi tatu muhimu dhidi ya Fulham baada ya mshambuliaji wao Papiss Cisse, kuwafungia bao pekee la mchezo huo kunako dakika ya 90 ya mchezo.

Ushindi huo umewawezesha Newcastle kuchupa hadi nafasi ya 13 kwa kufikisha pointi 36, hivyo kuzidi kujihakikishia kuwemo katika EPL msimu ujao huku Fulham wakibakia nafasi ya 10 kwa pointi 39

No comments:

Post a Comment