Pages

Saturday, January 26, 2013

SIMBA YAUA 3-1, AZAM NAYO YASHIKA KASI HUKU MTIBWA IKIPIGWA NA VIBONDE POLISI MORO

Wachezaji wa Simba wakimpongeza Ramadhan Chombo "Redondo" baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya tatu 
Mshambuliaji Mrisho Ngassa wa Simba  akiachia shuti huku beki Amani Kyata wa African Lyon  akijaribu kulizuia wakati wa mchezo wao wa ligi kuu uliochezwa leo uwanja wa Taifa
 
TIMU ya Simba leo imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa  kuichapa African LLyon mabao 3-1 katika mchezo wa ufunguzi wa duru hilo. uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
 
Hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyotiwa kimiani na Mrisho Ngassa dakika za 19 na 39 na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ dakika ya tatu ya mchezo huo.

Lyon walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31, baada ya Shamte Ally  kukosa penalti baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis aliyepanda kusaidia mashambulizi, na mkwaju huo kupangulliwa na Juma Kaseja, lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai kipa huyo alitoka kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.

Kipindi cha pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC wasiongeze mabao zaidi, huku wao wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Bright Ike dakika ya 59 akipokea pasi ya Fred Lewis.

Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar imefungwa bao 1-0 nyumbani na Polisi Morogoro, bao likifungwa na Muzamil Said dakika ya 76, Coastal Union imeifunga Mgambo JKT 3-1, Ruvu Shooting imeilaza JKT Ruvu bao 1-0 bao pekee la Abdulrahman Seif dakika ya 90, Azam FC imeshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na JKT Oljoro imeilaza Toto Africans mabao 3-1

Ushindi wa Azam umetokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 20 na Khamis Mcha dakika za 31 na 66, wakati la Kagera lilifungwa na Paul Ngway dakika ya 82 na sasa timu hiyo imejiimarisha katika nafasi ya pili kwa kutimzia pointi 27, sasa ikizidiwa pointi mbili na Yanga ambayo ipo  kileleni.

Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mabao ya Coastal yalifungwa na Philip Mugenzi dakika ya 18, Daniel Lyanga dakika ya 78 na Joseph Mahundi dakika ya 81, wakati la Mgambo lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 89.

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mabao ya Oljoro yalifungwa na Hassan Isihaka dakika ya 15, Paul Nonga dakika ya 51 na 57, wakati la Toto lilifungwa na Selemani Kibuta dakika ya 73.

Ligi hiyo itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapo onyeshana ubabe na TZ Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.

African Lyon; Abdul Seif, Fred Lewis, Jacob Massawe, Mohamed Samatta, Abdulaghan Gulam, Yussuf Mlipili, Jackson Kanywa, Aman Kyata, Job Ibrahim, Shamte Ally na Juma Seif ‘Kijiko’

No comments:

Post a Comment