Pages

Friday, January 25, 2013

MZUNGUKO WA PILI KUANZA KESHO, NANI ATAPANDA NINI NA NANI ATAVUNA NI MAPEMA?

Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa katika viwanja sita tofauti.

Mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka Oman kwenye ziara ya mafunzo

Pia Kocha wake mpya, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses Basena na Jamhuri Kihwelo.

Mwamuzi wa kimataifa Israel Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo African Lyon inatarajiwa kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya kusitisha kibarua cha Pablo Velez kutoka Argentina kutokana na kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Coastal Union ambayo kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo Mzimbabwe Tinashe Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Timu zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi.

Ni mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Maafande wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.

Yanga iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Vinara hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.

Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.

Wakati ameingiza wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha wa Tanzania Prisons, Jumanne Chale amempoteza David Mwantika katika dirisa hilo. Beki huyo ametua katika timu ya Azam.

                              Msimamo kabla ya mapumziko ulikuwa hivi

Rnk Team MP W D L GF GA +/- Pts
1  Young Africans 13 9 2 2 25 10 15 29
2  Azam 13 7 3 3 17 11 6 24
3  Simba SC 13 6 5 2 20 11 9 23
4  Mtibwa Sugar 13 6 4 3 18 12 6 22
5  Coastal Union 13 6 4 3 16 14 2 22
6  Kagera Sugar 13 5 6 2 15 10 5 21
7  Ruvu Shooting 13 6 2 5 19 17 2 20
8  Mgambo JKT 13 5 2 6 10 13 -3 17
9  JKT Ruvu 13 4 3 6 13 20 -7 15
10  JKT Oljoro 13 3 5 5 13 16 -3 14
11  Tanzania Prisons 13 3 5 5 8 12 -4 14
12  Toto African 13 2 6 5 10 15 -5 12
13  African Lyon 13 2 3 8 9 20 -11 9
14  Polisi Morogoro 13 0 4 9 4 16 -12 4

No comments:

Post a Comment