Pages

Thursday, December 20, 2012

ABIDAL JEMBE LA BARCELONA LILILORUDI UWANJANI

KLABU ya Barcelona, imethibitisha kuwa beki wake mzoefu, Eric Abidal atafanyiwa upasuaji wa kubadilishwa ini wiki chache zijazo.

Taarifa hii ambayo ilitolewa Machi 15 mwaka huu, itakuwa ikikumbukwa na kila shabiki wa soka hususan wa Barcelona, kutokana na kwamba kuna ambao walifikiria kuwa huenda ndio ulikuwa mwisho wa mchezaji huyo kuonekana uwanjani.

Upasuaji huo ulifanyika ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu afanyiwe upasuaji mwingine wa kuondoa uvimbe uliokuwa ndani ya kiungo hicho.

Taarifa za kufanyiwa upasuaji huo hazikuwa mbaya kwa mashabiki wa Barcelona tu, bali kwa kila mpenda soka ulimwenguni ambapo baada ya kutolewa taarifa hiyo ambayo Barcelona haikutoa ufafanuzi zaidi, kila mtandao wa kijamii ulijaa ujumbe wa kumtakia kila la kheri mchezaji huyo.

Mbali na kwenye mitandao kabla ya mechi za raundi ya 16 ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, wachezaji wote wa timu zote mbili za Real Madrid na Olympique Lyonnais, walivaa jezi zilizokuwa na  ujumbe wa kumtakia kila la kheri  Abidal.

Ujumbe huo pia ndio ulikuwa ukionekana pia kwenye ubao wa kuonesha idadi ya mabao katika uwanja ambao mechi hiyo ilipigwa wa Santiago Bernabeu, ikiwa ni sehemu ya kumuunga kumfariji   mchezaji huyo.

Kabla ya kufanyiwa upasuaji huo, Machi 28 mwaka jana katika mechi ya fainali za Klabu Bingwa Ulaya kati ya Barcelona na  Manchester United, ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, mchezaji huyo alicheza dakika zote 90 ikionesha kuwa alikuwa amepona.

Hali hiyo ndiyo iliyomfanya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Carles Puyol  kumkabidhi beji ya unahodha na kumruhusu kubeba kombe hilo mbele ya mashabiki 85,000 waliojazana kwenye uwanja wa Wembley jijini  London.

Aliruhusiwa kutoka hospitali Mei 21  mwaka huu na kuendelea kujiuguza nyumbani na madaktari baadaye wakatangaza kuwa anaweza kucheza tena soka katika kipindi kifupi kama atahitaji kufanya hivyo na Oktoba mwaka huu, mchezaji huyo akaanza kujifua kidogokidogo.

Lakini hata hivyo juzi mashabiki wa timu hiyo wamepata taarifa za kufurahisha zinazoeleza kuwa, 'jembe' lao muda wowote linaweza kuwa  limerejea kibaruani.

Taarifa zilizotolewa na Gazeti la Marca  juzi, zilieleza kuwa beki huyo alipewa hidhini na madaktari wa timu hiyo baada ya kuona anaendelea vizuri.

"Baada ya kupona vizuri tangu alipofanyiwa upasuaji, madaktari wameamua kuwa beki huyo wa kushoto wa  Barcelona na timu ya  Taifa ya Ufaransa yupo tayari kurejea katika mapambano yake ya ushindani wa soka," lilieleza  gazeti hilo likiwanukuu madaktari waliokuwa wakifuatilia hali ya afya yake.

Wakati taarifa hizo zikitolewa tayari Abidal, 33, alishaanza kujifua nje ya kikosi cha kwanza na kwamba kwa sasa anaweza kuwa chini ya usimamizi wa kocha wa kikosi hicho cha kwanza, Tito Vilanova, ingawa   hadi sasa tarehe maalum ya kurejea uwanjani haijafahamika, lakini inavyodhaniwa ni kwamba huenda Mfaransa huyo akashuka uwanjani kuanzia mapema mwezi ujao.

Abidal alisaini mkataba wa miaka minne wa kuitumikia Barcelona Juni  29 , 2007, ambao ulikuwa na thamani ya euro milioni  15.

Baada ya kusaini mkataba huo alikabidhiwa  jezi namba  22  tofauti na jezi namba  20 aliyokuwa akivaa katika timu ya  Lyon  kutokana na kwamba jezi hiyo tayari alishakabidhiwa  Deco.

 Mechi yake ya kwanza katika michuano  ya  La Liga,  ilikuwa ni  Agosti  26, 2007  ambayo timu yake ilitoka suluhu na timu ya Racing de Santander.

Alikamilisha msimu huo wake wa kwanza ambao Barcelona iliumaliza ikiwa katika nafasi ya tatu akiwa  amecheza  mechi 30 na aliikosa mechi ya fainali ya michuano ya KlabuBingwa Ulaya 2009 dhidi ya   Manchester United, baada ya kulimwa kadi nyekundu katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Chelsea, baada ya  kumfanyia madhambi  Nicolas Anelka  wakati akijiandaa kufunga bao.

Mbali na Barcelona pia taarifa hizo zitakuwa  za faraja  katika timu ya Taifa yaUfaransa  kutokana na mchango mkubwa ambao amekuwa  akiutoa katika timu hiyo.

Hadi anafanyiwa upasuaji  Abidal alishaichezea timu ya Taifa ya Ufaransa mechi 61  na tangu aoneshe uwezo wake katika mechi yake ya kwanza  ya kirafiki dhidi ya Bosnia na Herzegovina iliyopigwa Agosti 18, 2004 beki huyo amekuwa chaguo la kwanza kwa kila kocha anayekabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo .

No comments:

Post a Comment