Pages

Monday, October 1, 2012

YANGA YAIWINDA SIMBA DAKIKA 120

Kocha Ernust Brands wa Yanga akiwa na wachezaji baada ya kumaliza mazoezi


Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini leo huku kocha wao mpya Ernust Brands akifuatilia kwa makini

 

ZIKIWA zimebakia siku moja kabla ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga ambao ni wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baadhi ya mbinu za kutafuta ushindi zimekuwa zikiendelea kwa Wanajangwani.

Katika mazoezi ambayo, HABARI ZA MICHEZO  iliweza kuyashuhudia kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Yanga ilikuwa inanolewa na kocha mpya, Ernstus Brands ilikuwa ikitengeneza kikosi maalum cha ushindi ambacho kitashuka kesho kwenye uwanja huo huku kikiwa na damu mchanganyiko.

Baadhi ya wachezaji ambao waliweza kuonekana kupewa majukumu ni pamoja na Haruna Niyonzima,  Ally Mustafa ‘Barthez’, Oscar Joshua, Hamisi Kiiza, Athuman Idd Chuji, Saimon Msuva, Mbuyi Twite, Frank Domayo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,  Didier Kavumbagu  na Kelvin Yondani,  ambao walifanya mazoezi mepesi.

Yanga ambayo tofauti na siku nyingine ilikuwa imeimarisha ulinzi kwa kile kilichobainika kwamba ni kuhofia watani wao wa jadi kujua mbinu zao, ambazo zilikuwa zinatolewa na mholanzi huyo aliyejiunga na kikosi hicho akitokea APR ya Rwanda.

Aidha baadhi ya wachezaji walionekana kupewa majukumu ya ziada ya kupachika mabao ikiwa ni mikakati wa Ernstus Brands ya kuhakikisha anapata ushindi huku mfumo ambao aliokuwa anautumia ni pamoja na ule wa 4-4-2 na 3-3-4.

Mazoezi hayo yalifanyika kwa muda wa dakika 120 ambazo zilikuwa ni za nguvu hali ya juu inayoonyesha kwamba Mholanzi huyo anahitaji matokeo bora katika mchezo wa kesho.

Katika hatua nyingine, ulinzi ulikuwa ni wa hali ya juu kwenye mazoezi hayo ambapo hata mashabiki waliokuwa wanatarajia kuchungulia kupitia nondo zilizopo kwenye ukuta huo hivyo mashabiki hao kujikuta wakiambulia patupu.

Awali katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa juzi Jumapili, Yanga iliweza kushinda African Lyon kwa mabao 3-1 huku Kocha msaidizi, Fred Minziro akisema kuwa kazi iliyopo mbele yao ni kubwa.

“Tunajua kwamba tuna deni la kulipa mabao 5-0 ya msimu uliopita hivyo lazima tujitahidi na kuhakikisha kwamba tunapata ushindi ili tupate pointi 10 wakati wenzetu nao wanahitaji kushinda ili kusonga mbele zaidi.

“Kwa hali ilivyo ni lazima tujitume kadri inavyowezekana ili kuhakikisha tunawapa mashabiki wetu raha lakini najua nini cha kufanya ingawaje siwezi kuahidi mambo makubwa kutokana na mpira kuwa na matokeo matatu, kushinda, sare na kufungwa kwa hiyo lolote linaweza kutokea,” alisema Minziro.

Yanga kwa sasa ipo kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushuka dimbani mara nne huku ikishinda michezo miwili lakini imefanikiwa kupata sare moja na kufungwa mechi moja. Hadi sasa imefunga mabao saba na kufungwa matano ikiwa na pointi saba.



No comments:

Post a Comment