Pages

Monday, October 15, 2012

MWINTANGA AACHIWA HURU

Aliekua Rais wa shirikisho Ngumi za Ridhaa Tanzania (TBF) Alhaj Shaaban Mwintanga

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga, aliyeshitakiwa akidaiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Kuachiwa huru kwa Mintanga kunatokana na mahakama kueleza kuwa, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.

Jaji Dk. Fauz Twaib, alitoa uamuzi huo jana, kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani mbele yake ili kuamua endapo mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu au la. Alikuwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Jaji Twaib, upande wa mashitaka uliwasilisha mahakamani mashahidi wanne, ambao ni Christopher Mutarukwa, Nassoro Irenge, Emilia Poliano na Charles Ulaya.

Alisema ushahidi wa Ulaya umezua kuwepo kwa kujichanganya katika kesi ya upande wa mashitaka, ikiwemo uzito wa dawa za kulevya ambao kwenye hati ya kuonyesha thamani yake inaelezwa ni kilo 4.8 na kwenye kielelezo cha nukushi (fax) kutoka Mauritius inaonyesha ni kilo sita.

Jaji alisema ripoti kamili aliyopewa shahidi huyo hakuiwasilishwa mahakamani kama kielelezo na hakuna shahidi yeyote aliyetoa ushahidi kuhusu idadi ya kilo za dawa hizo.

Alisema tangu awali aliyekuwa akitafutwa kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo ni mtuhumiwa Mika na si Mintanga na kwamba, mtuhumiwa Msengwa ambaye anashikiliwa Mauritius kwenye maelezo yake alisema hamfahamu Mintanga.

Ulaya katika ushahidi wake alidai Msengwa alipatiwa dawa hizo na Mika katika hoteli iliyoko eneo la Manzese, Dar es Salaam na alikuwa akiwasiliana na mwanamke raia wa Kenya.

Jaji alisema upande wa mashitaka pia umeshindwa kuthibitisha mahali na tarehe ambayo washitakiwa walikula njama.

No comments:

Post a Comment