MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka amesajiliwa na klabu
ya Brighton & Hove
Albion FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake England.
Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo yenye makazi yake
Crawley, United Kingdom imemsajili Aisha
Masaka kutoka BK Hacken kwa masharti ambayo hayajawekwa wazi, kwa kuzingatia
taratibu za kawaida za udhibiti.
“Tunayofuraha kutangaza kumsajili mshambuliaji Aisha Masaka kutoka BK
Hacken kwa masharti ambayo hayajawekwa wazi, kulingana na taratibu za kawaida,”
alisema Zoe Johnson, Mkurugenzi Mkuu wa
soka la wanawake na wasichana, na kuongeza, "Tuna furaha kumkaribisha
Aisha, Brighton.
"Ameshindana kwa kiwango cha juu nchini Uswisi akiiwakilisha Hacken
kwenye Ligi ya Mabingwa (UEFA).
"Yeye ni mshambuliaji ambaye anatawala mpira na mfungaji wa asili.
Tunatazamia kumkaribisha Albion kabla ya msimu mpya.”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Hacken mwaka 2022
akitokea Yanga Princess na pia amewahi
kuichezea Alliance FC ya Mwanza.
Katika misimu miwili aliyokaa Hacken, aliwasaidia kumaliza nafasi ya pili
kwenye Ligi ya Uswisi na walifika robo fainali ya UEFA msimu uliopita kabla ya
kushindwa na PSG.
Katika kipindi chake cha Ligi Kuu ya Tanzania, alishinda mfungaji bora
katika kampeni za 2020/21 baada ya kuifungia Yanga Princess mabao 35 katika
mechi 20.
Katika ngazi ya kimataifa ameichezea Tanzania mechi 15, akifunga mabao tisa
tangu alipoanza kucheza mwaka 2021.
Kwenye michuano ya Kombe la COSAFA ya wasichana chini ya umri wa miaka 17
alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa na yeye kumaliza mfungaji bora.
Pia ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Tanzania kilichofuzu kucheza
michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake (AFCON 2024) itakayofanyika
Morocco mwakani baada ya kusogezwa mbele.
Masaka anakuwa mchezaji wa kwanza kwa
wanawake kucheza Ligi Kuu England lakini wa pili akitanguliwa na Mbwana Samatta
aliyecheza Aston Villa mwaka 2020.
Wachezaji wengine wa Twiga
Stars wanaocheza nje na klabu zao kwenye mabano ni Clara Luvanga (Al
Nassr- Saudia), Enekia Kasonga (Flames-Saudia), Julietha
Singano (Juavares - Mexico), Opah Clement (Beskitas - Uturuki), Diana
Msewa (Amed Spor - Uturuki) na wengine wanaocheza nchi za Afrika
Mashariki.
No comments:
Post a Comment