Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, September 13, 2017

TRA yaanza kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha kama ambavyo ilikabidhiwa jukumu hilo kuanzia Julai Mosi 2017 kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa kodi katika michezo hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Kayombo alisema kuwa TRA inakusanya mapato katika michezo mbalimbali ya kubahatisha hapa nchini kama vile Casino, Sport Betting, Slot Machines, Lottery na kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) na kusisitiza kuwa kiwango cha kodi kinatofautiana kati ya mchezo mmoja na mwingine.
“Jukumu hili limetokana na mabadiliko ya sheria ambayo yapo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 ambayo imetupa mamlaka kamili ya kusimamia zoezi la ukusanyaji wa mapato katika michezo ya kubahatisha,” alifafanua Kayombo.
Alibainisha kuwa kwa wanaojihusisha na michezo hiyo katika Casino wanapaswa kuwasilisha TRA asilimia 15 ya mapato yatokanayo na mchezo huo kwa wiki na wanaochezesha michezo ya Sport Betting wanatakiwa kuwasilisha asilimia 6.
Kayombo aliongeza kuwa kwa wale wanaochezesha michezo hiyo kwa njia ya SMS wanatakiwa kuwasilisha asimilia 30, kwa michezo ya kitaifa (National Lottery) wanatakiwa kuwasilisha asilimia 10 na michezo ya slot machine wanatakiwa kuwasilisha sh. 32,000 kwa mwezi kwa kila machine moja.
“Michezo ya kubahatisha ina pande mbili yaani mchezeshaji na mchezaji hivyo kila mmoja anapaswa kulipa kodi, ambapo mshindi wa mchezo huo pia anapaswa kulipa asilimia 18 ya mapato yake ambayo hukatwa na mchezeshaji na kuiwasilisha TRA,” alisema Kayombo.
Aidha Kayombo alieleza kuwa TRA itajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato tu, jukumu la kuratibu na kuendesha michezo hiyo litabakia kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha hapa nchini ambayo ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia michezo yote ya kubahatisha.
Alisema TRA inashirikiana na Bodi ya Michezo hiyo katika kutoa elimu kwa wadau wote wanaohusika na michezo ya kubahatisha wakiwemo wadhamini, wananchi, vyombo vya habari na wadau wengine.
Pia TRA imetoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wanaohusika na michezo ya kubahatisha kuendelea kutoa ushirikiano katika suala la ukusanyaji mapato yatokanayo na michezo hiyo kwa ufanisi zaidi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 kama ilivyopitishwa na Bunge.
Michezo ya Kubahatisha inasimamiwa na kuendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Board of Tanzania) ambayo mwanzoni ndiyo ilikuwa na jukumu la ukusanyaji kodi ambalo kwa sasa limerudishwa TRA kwa mujibu wa Sheria ya Fedha Na. 4 ya mwaka 2017 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuifanyia marekebisho.

No comments:

Post a Comment