NAHODHA wa
timu ya Taifa ya soka ya Wasichana (U-20) ‘Tanzanite’ Wema Richard amewaahidi Watanzania kurudi na
ushindi katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Dunia dhidi ya Nigeria
unaotarajiwa kuchezwa Abuja Jumamosi.
Hayo
aliyasema leo wakati akikabidhiwa bendera ya Taifa na Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Michezo wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Yusuph Singo
katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Karume, Dar es
Salaam.
Wema alisema
kikosi chao ambacho kipo chini ya kocha Sebastian Nkoma kimepata maandalizi ya
muda mrefu japo hawakupata mechi ya kirafiki ya kimataifa lakini wamejiandaa
kupambana ili warudi na ushindi.
“Kocha
amemaliza kazi yake kilichobaki na sisi wachezaji kuonesha kwa vitendo kile
tulichofundishwa na sisi tupo tayari kwa kazi na kauli mbiu yetu ni ‘kazi
kazi,” alisema Wema.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi bendera Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Dk. Yusuph Singo
aliwaambia wachezaji hao Watanzania wanapenda mpira hivyo wanategemea ushindi.
“Timu yenu
ni nzuri japo sijabahatika kuwaona mkicheza kama Tanzanite ila baadhi nimewaona
mkicheza kama Makongo, Mlandizi na timu nyingine lakini naamini mtakwenda
kufanya vizuri,” alisema Dk. Singo.
Pia Singo
aliwaambia wako sokoni hivyo wakacheze kwa kuonesha vipaji vyao kwani wanaweza
kupata timu za kucheza au kufanya majaribio kama ilivyokuwa kwa Serengeti boys.
Naye Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao alikiri timu hiyo kukosa michezo wa kirafiki
wa kimataifa lakini akasema TFF imejitahidi kuwalipa wachezaji hao posho zote
kuanzia walipoanza kambi.
“Kama TFF
tumetimiza wajibu kwa kuwalipa posho zote mnazodai na hata posho za nje mkuu wa
msafara atakabidhiwa kwani zipo tayari na nyie wachezaji pamoja na benchi la
ufundi mnakwenda kutimiza wajibu,” alisema Kidao
No comments:
Post a Comment