MTIBWA Sugar
imeendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya leo kutoka sare
ya bao 1-1 na Ruvu Shooting kwenye mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini,
Pwani.
Kwa matokeo
hayo Mtibwa Sugar wamefikisha pointi 10 baada ya kucheza michezo minne na
kushinda michezo mitatu huku nafasi ya pili Singida United ikiwa na pointi
tisa.
Ruvu
Shooting walitanguliaji kufunga bao dakika ya kwanza likifungwa na Zuberi Dabi lakini
dakika ya 25 mshambuliaji Stahimili Mbonde aliisawazishiwa Mtibwa Sugar.
Katika dimba
la Jamhuri Dodoma Singida United waliweza kuutumia vema uwanja wa nyumbani kwa
kuifunga Kagera Sugar bao 1-0, lililofungwa na Tafadzwa Kutinyu kwa penalti
dakika ya 89.
Huu ni
mchezo wa nne kwa Kagera Sugar, kikosi kinachonolewa na kocha kijana mzawa
Mecky Maxime kikipoteza.
Stand United
ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga iliifunga Mbeya City mabao 2-1, mabao ya Stand yalifungwa na Kisatya
Sahan dakika ya 53 na la pili lilifungwa
na Ally Ally dakika 62 na bao pekee la Mbeya City lilifungwa na Mohamed Samatta
dakika ya 57
Baada ya
kumalizika kwa mzunguko wa nne ligi inatarajiwa kuendelea tena Septemba 30
ambapo kutachezwa michezo saba na mchezo mmoja utachezwa Oktoba Mosi.
Baada ya
hapo timu ya Taifa ya soka itaingia kambini kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa
kimataifa dhidi ya Malawi unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 7 katika Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment