Maamuzi hayo magumu yanafuatia ripoti mbaya ya kamati maalum iliyotumwa nchini humo kukagua miundombinu ikiwemo ubora wa viwanja na hali ya usalama.
Licha ya viwanja vingi kutokuwa tayari na vingine kuwa chini ya kiwango, sababu nyingine iliyochagiza maamuzi hayo ni kutotengamaa kwa hali ya kisiasa nchini humo kufuatia mahakama kuu kuamuru uchaguzi wa Rais urudiwe.
Wiki hii wizara ya michezo ya nchi hiyo iliidhinisha kiasi cha shilingi za Kenya 4.2 bilioni kwa ajili kukamilisha ukarabati wa viwanja lakini inaonekana jambo hilo limekuja kwa kuchelewa.
CAF itatangaza upya nafasi ya kuandaa michuano hiyo kwa nchi ambazo zitakuwa tayari zina miundombinu itakayowezesha kufanyika kwa michuano hiyo miezi mitatu ijayo.
Mwaka 1996 Kenya ilipoteza nafasi ya kuandaa michuano ya AFCON kwa sababu zinazofanana na hizi. Badala yake michuano hiyo ilipelekwa Afrika Kusini ambao walitumia vizuri viwanja vya nyumbani kwa kutwaa taji hilo wakiwafunga Tunisia kwenye mchezo wa fainali.
Mapema Rais wa chama cha soka cha Kenya (FKF) Nick Mwendwa alisema atajiuzulu nafasi yake kama nchi yao itapokonywa haki ya kuandaa michuano hiyo. Wakenya wanasubiri kuona kama kigogo huyo atatimiza ahadi yake au atabadilisha mawazo.
No comments:
Post a Comment