Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, June 4, 2017

NELSON ISSANGYA:MTANZANIA ANAYETAMBA MAREKANI







“NINAISHI Marekani lakini mimi ni Mtanzania,” ni maneno ya mshindi wa tuzo tano za kutunisha misuli, Nelson Issangya ambaye anafanya shughuli zake nchini Marekani.

Issangya ambaye ni mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) anasema amezaliwa mkoa wa Arusha, wilaya ya Arumeru katika kijiji cha Sakila.

Issangya anasema alikwenda Marekani mwaka 2003 kusoma shahada ya Computer and Information Systems na baada ya kuhitimu alipata kazi ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) huko huko Marekani.

“Baada ya kwenda Marekani mwaka 2003 nilijiunga na chuo ambapo nilitunukiwa shahada yangu ya Computer and Information Systems,” anasema Issangya.

Kijana huyo ambaye ni mpole huku akiongea taratibu anasema alivutiwa na mchezo wa kutunisha misuli na kuamua kujifunza na kujikuta akifanya vizuri.

“Mbali na kushindana kwenye mashindano ya kutunisha misuli,  ninafanya kazi kama mtaalamu wa mawasiliano, hivyo mchezo huu naufanya baada ya kazi,” anasema Issangya.
Kwa sasa ameshajinyakulia tuzo tano katika mashindano mbalimbali aliyoshiriki na kusema kila shindano analoshiriki anajitambulisha kuwa ni Mtanzania.

“Marekani ninaishi katika jimbo la Oregon tangu nimewasili na mazoezi nimeanza kufanya toka nilipowasili  wakati nasoma. Mwaka 2015 ndio nilianza kushiriki mashindano mbalimbali ya kutunisha misuli,“ anasema.

Issangya anasema ameshinda tuzo mbili za mashindano ya Jimbo la Oregon State, Cascadian Classic katika Jimbo la Oregon na tuzo mbili za Emerald Cup, katika Jimbo la Washington State.

Anasema changamoto anazokutana nazo katika mchezo huu ni jinsi ya kugawa muda wake wa mazoezi na kazi yake ambayo ni ya kuajiriwa.

“Mimi ni mwajiriwa na kufanya mazoezi ili kushindana ni changamoto inayonikabili katika mchezo huu, lakini najitahidi kufanya mazoezi ya nguvu katika muda kidogo ninaopata,”  anasema.

Anasema malengo yake katika mchezo huu ni kujifunza kadri awezavyo  baadae aweze kuwa kocha au mkufunzi atakaporejea nchini Tanzania.

“Ninataka kujifunza kadri niwezavyo kwani baadaye nitapenda sana kuelimisha watu hasa Tanzania jinsi ya kufanya mazoezi na kula vizuri ili kujenga misuli,” anasema.

Issangya anasema hajulikani na Chama cha Watunisha Misuli cha Tanzania wala kikundi chochote kinachofanya mchezo huo,  licha ya yeye kujitambulisha katika mashindano yote kuwa ni Mtanzania.

“Napenda Watanzania wafahamu kuwa kuna kijana wao anaitwa Nelson Issangya anayewatangaza kupitia mchezo huu hivyo kama kuna Chama cha Watunisha misuli Tanzania ningependa kuonana nao,” anasema.

Pia kupitia makala haya anaowamba wale wanaopenda mchezo huu wawasiliane kupitia ukurasa wake wa facebook wa Nelson Issangya.

Anasema anatamani siku moja Tanzania iwe na mashindano mengi kama ilivyo Marekani, ambapo mashindano yapo ya kila aina na kila jimbo hali inayomfanya mshiriki kuchagua sehemu anayotaka kushiriki.

Issangya alipata elimu ya msingi katika shule ya Sakila  na baada ya kuhitimu alijiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Makumira.

Baadae alisoma ufundi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Dar es Salaam, baada ya kuhitimu elimu ya ufundi alirudi Arusha na kusoma kozi ya kiingereza na Tour Guide katika Chuo cha Mount Meru.

No comments:

Post a Comment