Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, May 10, 2017

TFF YAVITAHADHALISHA VYOMBO VYA HABARI KUACHA KAMPENI CHAFU
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limevitaka baadhi ya vyombo vya habari nchini kuacha kampeni za upotoshaji zenye lengo la kuwachafua viongozi wa juu wa shirikisho hilo.
Akizungumza na wandishi wa habari Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema TFF imeshtushwa na taarifa inayoendelea kutolewa kwenye gazeti moja la kila siku ikidai kuwa kuna ufisadi ndani ya shirikisho wakati madai hayo ni ya uongo na yenye lengo la kujenga mtazamo hasi dhidi ya shirikisho na viongozi wake.
“Gazeti hilo la kila siku limetumia taarifa ya ukaguzi wa fedha iliyofanywa na wakaguzi kutoka TAC kujenga picha kuwa ni ushahidi tosha wa kuwepo kwa ufisadi ndani ya shirikisho,” alisema Lucas.
Pia Lucas alisema taarifa ya ukaguzi wa fedha ya TAC haikuwahi kuituhumu TFF kwa ufisadi bali ilibaini maeneo ya kiuhasibu ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya namna baadhi ya malipo yalivyofanyika na ufafanuzi ulitolewa kwa ufasaha na watendaji wa shirikisho na kupelekwa kwennye Mkutano Mkuu wa Shirikisho.
 Aidha Lucas alisema hata hivyo gazeti hilo ambalo limeonekana kuweka kando kabisa misingi ya uandishi wa habari, limechapisha taarifa bila hata kutoa nafasi kwa wanaotuhumiwa kujibu na kutoa ufafanuzi stahiki.
 “Rais na katibu mkuu wa shirikisho wanahudhuria mikutano ya CAF nje ya nchi wakati gazeti hilo likiendelea kuporomosha mlolongo wa tuhuma bila kutoa haki ya kusikilizwa kwa wanaoandikwa vibaya,” alisema Lucas. 
TFF inaliangalia suala hili kama kampeni chafu inayofanywa ili kushawishi matokeo ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
 Lucas alisema taarifa hii potofu inalenga kulihamisha taifa kutoka kwenye masuala ya msingi kama kuiunga mkono Serengeti Boys kwenye mashindano ya Afrika na kuanza kujadili masuala yanayohusiana na siasa za uchaguzi wa TFF.
TFF inatafakari hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya vyombo vya habari husika na inachukua nafasi hii kuvisihi vyombo vya habari kuacha mara moja kujihusisha na kampeni ya kuchafuana ambayo ni kinyume na misingi ya maadili ya uandishi wa habari.