TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17,
Serengeti Boys jana ilianza vema michuano ya Afrika baada ya kuwabana mabingwa
watetezi, Mali na kutoka nao suluhu.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Stade de l’Amitie mjini Libreville, Gabon
Serengeti Boys ilianza kwa mashambulizi ya harakaharaka dakika za mwanzo za
kipindi cha kwanza hali iliyowachanganya wachezaji wa Mali.
Timu hiyo inayoshiriki michuano hiyo ya Afrika kwa mara ya kwanza
ilionekana kutotetereka dhidi ya mabingwa hao watetezi ambapo wachezaji wake
walicheza kwa kujiamini zaidi mpaka mwisho wa mchezo huo huku safu yake ya
ulinzi ikionekana kuwa imara zaidi.
Serengeti, ambayo sasa ina pointi moja, inajiandaa kucheza na
Angola keshokutwa mechi ambayo ina nafasi ya kushinda.
Wawakilishi hao watacheza mechi ya mwisho Jumapili ya wiki hii
dhidi ya Niger.
Timu nne za juu kwenye michuano hiyo zitafuzu kucheza fainali za
kombe la Dunia kwa vijana zilizopangwa kufanyika India Oktoba mwaka huu, na
hilo ndilo lengo la Serengeti Boys.
Akizungumza kwa njia ya simu muda mfupi baada ya mechi ya jana,
kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime aliwashukuru wachezaji wake kwa kujiamini
katika mechi hiyo.
“Sasa hizo mechi
nyingine zitakuwa rahisi kwetu kwa sababu tulichokuwa tunakitaka ni kutofungwa
na bingwa mtetezi, vijana wetu wamejitahidi sana, Watanzania waendelee
kutuamini tu,” alisema.
No comments:
Post a Comment