Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, May 29, 2017

ARTURO VIDAL: Mwana masikini anayechezea pesa



Image result for Arturo Vidal
*Babaye chapombe alichoma kitanda cha mama
ARTURO Erasmo Vidal Pardo, maarufu zaidi kwa jina la Arturo Vidal ni kiungo wa Bayern Munich.
Alizaliwa miaka 28 iliyopita Santiago, Chile katika lindi la umasikini, akakuzwa kwa shida sana lakini sasa anaogelea kwenye kiasi kikubwa cha fedha.
Hapana ubishi kwamba Vidal ni mmoja wa viungo mahiri kabisa duniani, akiwa amehudumu kwenye klabu kubwa kama Munich, na kabla ya hapo Juventus na Bayer Leverkusen.
Aliwindwa na Manchester United kiangazi cha mwaka jana, lakini kocha Louis van Gaal akawa na hofu juu ya utimamu wake wa mwili na kuumia mara kwa mara. Arsenal walihusishwa naye sana kiangazi hiki lakini amekwenda Allianz Arena.
Vidal ameshaanza kung’aa akiwa na Bayern na kama kuna kinachoonekana ni kuhatarisha namba ya Thomas Muller kwa sababu anaelekea kumudu zaidi na tayari ameifungia timu yake hiyo mpya.
Wazazi wake walikuwa watu wa hali ya chini na alikua katika hali ya ‘bora liende’ na kama si kugundulika kwa kipaji chake cha soka, huenda leo angekuwa chokoraa.
Akiwa mtoto alianzia timu ya Melipilla kabla ya kuingia kikosi cha vijana cha timu hiyo ya kwao, akaonekana na Colo-Colo, klabu iliyofanikiwa zaidi Chile, akaingizwa kwenye mfumo wao wa vijana.
Mwaka 2005 aliingizwa rasmi kwenye kikosi cha wakubwa, lakini akadumu kwa miaka miwili tu, kwani Bayer Leverkusen walimwona na kumdaka hadi 2011 alipochukuliwa na Juventus na mwaka huu Bayern.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile ameonesha kiwnago kizuri cha soka dimbani, lakini pia utovu wa nidhamu, pengine kutokana na asili ya alikokulia au tu kwa sababu ya ‘kunuka’ fedha ambazo pia huzichezea kwa anasa.
Akicheza sambamba na Alexis Sanchez wa Arsenal, Vidal alifanikiwa kuwapa Chile ubingwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 99, chini ya kocha Jorge Sampaoli.
Mwana huyu mkubwa wa mama Jacqueline Pardo na baba Erasmo Vidal alipewa jina kwa heshima ya babu yake aliyekufa ajalini wakati akiendesha gari la taka.
Nyumbani kwao kulikuwa na usumbufu mwingi kwa sabau ya wingi wa watu, bibi aliyekuwa hawezi tena kutembea na upungufu wa mahitaji, ikiwa ni pamoja na chakula.
Akiwa na umri wa miaka mitano, babaye aliyekuwa chapombe alikuwa akiuza mboga katika soko la La Vega, ambapo baada ya kuupiga mtindi alitia moto kitanda cha mama yao.
Baba huyo alifukuzwa na baadaye Vidal akatokea kuwa kama baba wa nyumba, huku mama yake mzazi akifanya kazi ya usafi kwa watu.
Tangu akiwa na umri wa miaka tisa, Vidal alikuwa akikwepa shule na baada ya utoro wake huo alikuwa akinyomga baiskeli yake kwa maili sita hadi Santiago kulikokuwapo na mbio za farasi.
Alikuwa na kazi kubwa ya kuwalisha na kuwapanga inavyotakiwa kutoka kwenye mashikizo yao, lakini huku akiwa makini kuchunga kiasi kidogo cha fedha alichokuwa akikusanya ili kisije kuibwa au kupotea.
Alishiriki pia katika kamari kwamba ni farasi yupi angeshinda mbio hizo; akipata ushauri wa mkubwa mmoja kumsaidia kuweka dau la nani angeshinda wakati familia na rafiki zake walimsubiri katika Jumuiya ya San Joaquin.
Binafsi alipenda kushiriki mbio za farasi lakini alikuwa na wasiwasi iwapo angeweza; hivyo aliendelea na kazi ya kuwatunza.
Hata hivyo, bosi wake, Enrique Carreno, alipata kumwona akicheza na mpira pembezoni siku moja na alimwambia hivi juu ya farasi na mbio zake.
“We mwana, mchezo huu wa farasi haukufai, maisha yako ya baadaye ni kwenye soka,” alimwambia na tangu hapo Vidal akaongeza mazoezi.
Alipofikisha umri wa miaka 15, Vidal alimwahidi mamaye kwamba angekuja kumfanya kuwa malkia na kwamba hangefanya tena kazi za hovyo wala kuishi maisha ya shida.
Na kweli, maneno yake yalikuja kutimia alipoingia kwenye soka, akamjengea nyumba nzuri na zaidi ya hapo alikuwa na hamu ya kusoma, akaenda masomoni.
Moja ya tatuu zake ipo moja ya mbio za farasi, nyingine yenye sura ya mama yake iliyo chini kidogo ya bega lake la kulia.
“Mama alifanya kazi ngumu sana. Huwa namsaidia kwa kila ninaloweza na najihisi kuwajibika pia kwa wadogo zangu. Nilianza zamani sana kazi ya ‘ulezi’ kwa sababu nilikuwa kama baba nikiwa bado mtoto na napenda sana kuhusishwa na hali hiyo,” anasema Vidal.
Baba yake alijaribu kujiua mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na 2008 baada ya kuchapa mtindi aina ya Pisco ambayo ni wiski.
Miaka mitatu baadaye alikamatwa sambamba na dada yake wakidaiwa kujihisisha na usafirishaji mihadarati baada ya polisi kumkamata akiuza kokeini.
Baba mkubwa wa Vidal aitwaye Ricardo ambaye hakuwa na makazi zaidi ya kuishi mitaani kwenye viambaza vya majumba ya watu alikuwa mlevi wa kupindukia na alifariki dunia miaka miwili iliyopita.
Wakati akiitunza familia yake ndipo bosi wake kwenye mbio za farasi akagundua kipaji chake cha soka na akawa anacheza mchangani karibu na klabu ya Kanisa Katoliki ya Rodelindo.
“Daima ungemwona akiwa na mpira wa miguu, aliupenda sana, alilala nao, akaamka nao, akacheza kabla na baada ya shule, aliporudi nyumbani kwa chakula cha mchana na baada ya kuacha shule,” anasema mjomba wake, Victor.
Vidal alikuja kupachikwa jina la utani la 'Cometierra' ambalo maana yake ni ‘mla vumbi’ kutokana na jinsi alivyochafuka kila mahali kwa vumbo kwa sababu ya mchezo wake na hadi leo ameshikilia mtindo huo wa kucheza.
“Tulijua angekuja kuwa mchezaji mzuri sana, tulimuunga mkono kwa hilo na sasa tunafurahia,” anasema kiongozi wa klabu hiyo ya Kanisa na rafiki wa familia yake, Ramon Henriquez.
“Alipenda kusema kwamba anataka kwenda kuionesha dunia uwezo wake na kwamba angekuwa mchezaji wa kulipwa. Na kweli, amekuja kucheza na magwiji kama Gianluigi Buffon na Andrea Pirlo,” anasema.

No comments:

Post a Comment