Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, December 28, 2016

YANGA YAMALIZIA HASIRA KWA NDANDA, YAIFUNGA 4-0






Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wamewapoza mashabiki wake baada ya kuichapa Ndanda FC mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kupunguza idadi ya pointi kutoka nne hadi moja dhidi ya vinara Simba.

Yanga wamefikisha pointi 40 wakiwa nafasi ya pili ambapo alama hizo zinaweza kuongezeka na kurudi nne za awali endapo Simba atashinda mchezo wake wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa uwanjani hapo kesho.

Mashabiki wa timu hiyo waliwatolea maneno makali wachezaji wa mabingwa hao katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao moja dhidi ya African Lyon Ijumaa iliyopita kwa madai walifanya kusudi kupata matokeo hayo ili kushinikiza uongozi kuwalipa mishahara yao iliyochelewa mwezi Novemba.

Katika dakika 25 za kwanza Yanga walikuwa tayari wamefunga mabao matatu kupitia kwa Donald Ngoma aliyefunga mawili dakika ya nne na 21 huku Amissi Tambwe akifunga la tatu na kuwafanya mabingwa hao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo.
Dakika ya 60 kocha Lwandamina alimuingiza kiungo Justine Zulu ambaye alionyesha umahiri mkubwa wa kupiga pasi na kukaba hali iliyoibua shangwe kila alipogusa mpira.

Beki Vicent Bossou aliifungia Yanga bao la nne dakika ya 88 kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Juma Abdul.

Kocha wa Ndanda Hamimu Mawazo aliwapumzisha Salvatory Ntebe na Abuu Ubwa na kuwaingiza Ayoub Shabani pamoja na Salum Minely.

Kwa upande wa Yanga iliwatoa Saidi Makapu, Haruna Niyonzima na Emmanuel Martin nafasi zao zikachukuliwa na Zulu, Thaban Kamusoko pamoja na Deus Kaseke.

No comments:

Post a Comment