Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, October 14, 2016

SIMBA KUENDELEZA UBABE KESHO?WEKUNDU wa Msimbazi Simba na Chama la wana Stand United kesho  wanatarajiwa kuendeleza ubabe  katika viwanja viwili tofauti, kusaka pointi tatu zitakazowapa nafasi ya kuendelea kuongoza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba itakuwa Uwanja wa Uhuru  ikiikaribisha Kagera Sugar huku Stand United ikiwa ni mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga. Hizi ndizo timu zinazokimbizana kwa pointi hivyo, macho yote yataelekea kwao.
Simba ndio vinara wa ligi kwa pointi 20 katika michezo nane waliyocheza, wakijivunia kutopoteza mchezo tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Timu hiyo ya Msimbazi huenda ikaendeleza ushindi baada ya kutoka kuifunga Mbeya City mabao 2-0 ugenini, kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya Jumatano.
Lakini pia, Kagera Sugar haiko katika kiwango kibaya msimu huu, kwani inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 15 katika michezo tisa iliyocheza.
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema anataka kuvuruga sherehe za Simba kwa kuhakikisha wanainyamazisha.
Licha ya tambo za wenyeji, itakumbukwa msimu uliopita Simba ikiwa katika kiwango kibaya iliifunga Kagera Sugar, ambayo nayo ilikuwa kiwango kibaya bao 1-0.
Mchezo huo huenda ukawa mgumu, kwani Simba itataka kushinda ili kuendelea kubaki kileleni, na Kagera inataka ushindi iendelee kuwa katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo yenye jumla ya timu 16.
Aidha, kama ilivyo kwa Simba hata Stand United imekuwa ni bora ikijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja. Leo itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa CCM, Kambarage Shinyanga.
Timu hiyo msimu huu imekuja kivingine baada ya kuwapiga vigogo wawili kwenye uwanja huo, yaani Yanga na Azam zote zikifungwa bao 1-0 kila moja.
Hio ndio timu inayoifukuzia Simba kwa pointi 19 hivyo, ni lazima itapambana kuendelea kulinda nafasi yake. Inakutana na timu ambayo ambayo iko katika kiwango cha kawaida ikiwa na pointi tisa katika michezo tisa.
Pia, Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tano kwa pointi 14 nayo itaendelea kusaka ushindi kwenye Uwanja wa Manungu dhidi  ya Tanzania Prisons ambayo nayo, haiko vizuri sana msimu huu, ukilinganisha na msimu uliopita.
Tanzania Prisons inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 10 katika michezo nane iliyocheza.  Timu zote mbili zinahitaji ushindi kwani  atakayepoteza atakuwa kwenye uwezekano wa kushuka kutoka nafasi moja hadi nyingine.
JKT Ruvu na Mwadui zitakutana zote zikiwa haziko katika nafasi nzuri. Mwadui ina pointi nane katika michezo nane ikishika nafasi ya tatu kutoka mwisho, na JKT Ruvu inashika nafasi ya nne kutoka mwisho ikiwa na point inane sawa na Mwadui.
Kila mmoja anahitaji ushindi kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja. Vile vile, Majimaji ambayo inashika mkia itakuwa ugenini dhidi ya Toto African kwenye uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza.
Timu hiyo ina pointi tatu ikishika nafasi ya mwisho, ikifuatiwa na Toto inayoshika nafasi ya pili kutoka mwisho ikiwa na point inane, wote wakiwa wamecheza michezo tisa.