Chama cha soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimezipongeza timu za taifa za soka, Kilimanjaro Queens iliyofanikiwa kuunyakua ubingwa wa michuano ya Cecafa ya wanawake iliyofanyika mjini Jinja nchini Uganda.
Timu hiyo iliyoiwakilisha Tanzania Bara na ikiwa chini ya
kocha mkuu Sebastian Nkoma na msaidizi wake Edina Lema,ilianza mashindano hayo
kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ambapo
imeisambaratisha Kenya kwa kuifunga mabao 2-1.
Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo amesema kitendo cha
Kilimanjaro Queens kutwaa kikombe hicho kinaonyesha ni kwa kiasi gani walivyo
tayari kwa ajili ya mapambano,na endapo nguvu kubwa itatumika katika maandalizi
yao wanaweza kulitangaza zaidi taifa lao.
Mbali na timu hiyo ya wanawake, DRFA imeimwagia sifa
Serengeti Boys inayosaka tiketi ya kutinga katika michuano ya kuwania kombe la
mataifa ya afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika mwezi
Aprili nchini Madagascar.
Kikosi hicho chini ya kocha Bakari Shime, kimebakiza mchezo
mmoja wa marudiano dhidi ya Congo Brazzaville kabla ya kutinga katika fainali
hizo,ambapo katika mchezo wa kwanza wamefanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-2.
Mwenyekiti Kasongo ameongeza kuwa mafanikio ya vikosi hivyo
vya taifa ni ya watanzania wote na kuwaomba wachezaji wasibweteke na hali hiyo
na badala yake wazidi kujituma ili kuboresha viwango vyao vya kucheza soka na
kulisaidia taifa.
IMETOLEWA NA DRFA.
No comments:
Post a Comment