Mshindi wa mbio za Mita 3000 katika kuruka viunzi na maji kutoka nchini Kenya, Ezekiel Kemboi, amenyang`anywa medali yake ya shaba aliyoishinda mjini Rio De Janeiro huko nchini Brazil.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34 aliyemaliza katika nafasi ya tatu na kutunukiwa medali ya Shaba katika mbio hizo.
Kilichosababisha Kenya kupokonywa medali hiyo ni baada ya Timu ya Ufaransa kukata rufaa mara baada ya kubainika kwamba mwanariadha huyo wakati mmoja anaruka kiunzi na maji alikanyaga nje ya mstari wakati akishiriki mbio hizo siku ya Jana.
Mfaransa Mahiedine Mekhissi alimaliza katika nafasi ya nne na amepandishwa hadi nafasi ya tatu na kupewa medali ambayo alikuwa amepewa Kemboi hapo awali.
Kemboi aliyeshinda katika Olimpiki za London 2012 katika michezo ambayo Mahiedine alishinda Fedha tayari ametangaza kwamba atastaafu riadha kutokana na umri wake.
Katika mbio hizo za jana mshindi alikuwa Mkenya Conseslus Kipruto ambaye pia aliweka rekodi mpya ya Olimpiki kwa muda wa dakika 8: 03.28 huku Mmarekani Evan Jager akimaliza katika nafasi ya pili kwa dakika 8: 04.28 na muda wa Kemboi ulikuwa dakika 8: 08.47 na Mekhssi alikuwa dakika 8: 11.52