Shauku ya wanachama na mashabiki wa Simba SC ya kuona klabu yao ikifanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ambao utamwezesha Mkurugenzi na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji MO kufanya uwekezaji katika klabu hiyo kongwe nchini sasa umefanikiwa.
Katika taarifa ambayo imetolewa na msemaji wa Simba, Haji Manara kuhusu mazungumzo yaliyofanywa na kamati ya utendaji ya Simba na Mohammed Dewji MO imeeleza kuwa kamati ya utendaji ya Simba kwa pamoja na MO wamefikia makubaliano ya kufanya mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu kuwa wa hisa.
“Kamati ya Utendaji ya Simba na Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Ltd imefikia imeafiki kuwepo mfumo wa uendeshwaji wa klabu kwa njia ya hisa,” alisema Manara.
Manara alisema kamati imefikia maamuzi hayo kwa kutambua kuwa uendeshwaji wa Simba unahitaji pesa nyingi ili klabu iwe na uwezo wa kushindana na vilabu vingine vikubwa Afrika na kutokana na MO alivyojieleza na mapenzi yake kwa Simba wameona ni sahihi kukubaliana na maeezo yake ili kuhamia katika mfumo wa hisa.
“Kimsingi pesa nyingi zinahitajika kuendesha klabu kama Simba ili niwe na uwezo wa kununua wachezaji wazuri, viwanja, majengo na hatimaye iwe na ubavu wa kushindana na timu zingine kubwa Afrika na si Tanzania pekee,
“MO alieleza kuwa yeye ana mapenzi na Simba na anayafanya haya kwa mapenzi ya klabu yake na si kwa nia nyingine … aliufahamisha mkutano kuwa hisa zitauzwa kwa wanachama wapya kwa taratibu makhususi na pia atawagaiya wanachama wa zamani hisa za bure,” alisema Manara.
Aidha Manara alisema kuwa kukamilika kwa mchakato mzima wa kufanya mabadiliko ya mfumo utatumia miezi sita na kwa kipindi hicho wanachama wa Simba watapatiwa elimu kuhusu mfumo mpya ili kila atakayenunua hisa atambue haki na wajibu wake katika mfumo mpya wa hisa
Pamoja na hayo, Manara alisema MO alikubali kuendelea kuisaidia Simba kama alivyokuwa akifanya kwa miaka iliyopita wakati wakifanya utaratibu mzima wa klabu kufanya mabadiliko ya mfumo na kuingia katika mfumo wa hisa ambao utakuwa tofauti na mfumo unaotumika sasa.
DSC_0136
DSC_0137 
kwa hisani ya MO blog