WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema serikali inawakaribisha wadau kuwekeza kwenye
michezo makao makuu ya nchi Dodoma.
Nape aliyasema hayo wakati
akikabidhiwa uwanja wa Uhuru na kampuni ya BCEG Ltd ambayo walikuwa wanaufanyia
marekebisho ya kuuboresha na kuufanya kuwa wa kisasa.
"Mimi kama waziri mwenye
dhamana ya michezo nawakaribisha wadau kuwekeza kwenye michezo hasa Dodoma
ambapo serikali inahamia pia nawataka wadau kuutunza uwanja huu na kulipa ada
za kuutumia", alisema Nape.
Pia Nape aliipongeza Azam kwa
kumiliki uwanja wao huku akiziasa Simba na Yanga kukamilisha taratibu za ujenzi
wa viwanja vyao ambao wamesema wanajenga.
Awali akikagua uwanja huo, Nape
aliwaonyesha wandishi wa habari eneo ambalo serikali imetenga kwa ajili ujenzi
wa ofisi wa vyama vya michezo kama walivyoomba kwa waziri mkuu alipokutana na
kuzungumza na viongozi wa vyama vya michezo mara baada ya kuingia madarakani.
"Eneo hili michoro yake ipo
tayari na lina ukubwa wa mita za mraba 4000 hivyo viongozi wanaweza kuja
ofisini ili kupewa michoro wajenge kwa gharama zao, eneo hili ni kubwa kwani
linaweza kujengwa baadhi ya ofisi za wizara", alisema Nape.
Awali akizungumza kabla ya
kukabidhi uwanja huo, Meneja wa BCEG Ltd, Cheng Longhai, alisema uwanja huo
ulianza kujengwa Mei 2015 na umegharimu bilioni 12.
Pia aliishukuru serikali kwa
uaminifu na ushirikiano walioipa kampuni yake tangu kuanza kazi na kukamilisha.
Baada ya kukabidhiwa uwanja wa
Uhuru, Nape alikwenda kukagua ujenzi wa mashine za elektroniki, uwanja wa Taifa
kukiri kuridhishwa kazi na kasi ya mashine zenyewe kwani zitakuwa zinatumia
sekunde 2 kwa mtu mmoja.
"Kazi hii inafanya na
serikali na hii inatokana na ahadi ambayo niliitoa ya kudhibiti mapato ya
kwenye michezo, kazi hii chini ya kampuni ya Selcom inaendelea vema na Septemba
4 watakabidhi rasmi", alisema Nape.
Pia Nape aliwatoa wasiwasi
mashabiki kuhusu umeme kwenye mashine hizo kwani zimefungwa UPS ambayo inaweza
kuhifadhi umeme zaidi ya saa tano lakini pia akawataka kujenga tabia ya kuwahi
kuingia uwanjani kuepuka msongamano.
Jumla ya mashine 20 zinatarajiwa
kufungwa Uwanja wa Taifa, 12 zitafungwa mageti ya mbele maarufu kama geti la
Simba, mashine 6 na geti la Yanga mashine sita na mashine nane zitafungwa
mageti ya nyuma kutokea uwanja wa ndani wa Taifa.
No comments:
Post a Comment