Katika siku za hivi karibuni,
kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu wakiwemo
wasanii watu wengine mmoja mmoja kutumia mavazi yanayofanana na sare za Majeshi
ya Ulinzi na usalama hapa nchini likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao
za kisanii au katika kazi mbalimbali, Jambo ambalo ni kinyume cha sheria,
kanuni na taratibu za Nchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa
ya Jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178
(1) na (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya
sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha wazi kuwa ni kosa
kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama
kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila
kibali kutoka kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia kitendo kilichofanywa
na kundi la kisanii la “ Original Comedy” kuvaa mavazi yanayoshabihiana na sare
za Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam
linachukua hatua za kisheria dhidi ya wasanii hao.
Aidha Jeshi la Polisi nchini, linatoa
onyo kali kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia mavazi yanayofanana
na sare zinazovaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini na
atakayebainika hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale
wote wenye mavazi yanayoshabihiana na sare za majeshi ya ulinzi na usalama
kuzisalimisha mara moja katika vituo vya Polisi vilivyokaribu nao.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu
No comments:
Post a Comment