NI kama gari inayopata pancha huku dereva akikaribia
kufika safari yake. Ndivyo ilivyotokea kwa Yanga le ilipotema kombe la
kwanza baada ya kufungwa na Azam kwa
mikwaju ya penalti 4-1 katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyofanyika kwenye uwanja
wa Taifa Dar es Salaam.
Ikiwa imeshahesabu ushindi baada ya kuongoza kwa
mabao 2-1 katika dakika 90 za mchezo huo, Yanga ilijikuta matatani baada ya
Azam kusawazisha bao dakika ya 90 na kulazimika kwenda kwenye mikwaju ya penalti
baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
Mechi hiyo ni ya kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa
Ligi Kuu bara ambayo msimu huu wa mwaka 2016/2017 unaanza keshokutwa.
Yanga imetema kombe hilo ililolitwaa mwaka jana
baada ya kuifunga Azam kwa mikwaju ya penalti 8-7. Timu hiyo bado inashikilia
ubingwa wa kombe la FA na wa Ligi Kuu.
Wachezaji Ramadhan Kessy aliyecheza Yanga kwa mara
ya kwanza na Haruna Niyonzima ndio waliokosa penalti ambapo Kessy penalti yake
kuokolewa na kipa wa Azam Aishi Manula huku Niyonzima kupiga juu. Kipa wa Yanga
Deogratius Munishi ‘Dida’ ndiye aliyepata penalti kwa upande wa Yanga.
Penalti za Azam zilifungwa na Bocco, Himid Mao,Kapombe na Michael Balou.
Yanga ilianza kwa kasi mechi hiyo na ilionekana kuwa
na kila dalili ya kuibuka na ushindi hasa baada ya Azam kuonekana kutojiweza
karibu dakika zote za kipindi cha kwanza.
Mshambuaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma
aliindikia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 18 kwa mkwaju wa penalti
iliyotolewa na mwamuzi Ngole Mwangole wa Mbeya baada ya Ngoma kufanyiwa
madhambi eneo la hatari na Shomari Kapombe.
Dakika moja baadae Ngoma aliandika bao lingine baada
ya kuunganisha krosi ya Amisi Tambwe na kuujaza mpira wavuni.
Bao hilo lilizidi kuwachanganya Azam ambapo sasa
wachezaji wake walionekana kupoteana zaidi lakini walihimili kwenda mapumziko
wakiwa nyuma kwa mabao hayohayo.
Azam ambayo haikupewa nafasi kubwa kushinda mechi ya
jana kutokana na kukosa matokeo mara kwa mara wanapokutana na Yanga, ilianza
kipindi cha pili kwa mabadiliko ambapo walimtoa Shaaban Chilunda na Ramadhan
Singano na nafasi zao kuchukuliwa na Francisco Zekumbariwa na Mudathir Yahaya,
mabadiliko yaliyoonekana kuzaa matunda kwani sasa ilibadilika na kuanza
kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Yanga.
Dakika ya 75 Kapombe aliisawazishia Azam bao la
kwanza baada ya kuunganisha pasi ya Jean Mugiraneza na kuujaza mpira wavuni.
Dakika ya 90 John Bocco aliisawazishia Azam bao la
pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi baada ya beki wa Yanga
kushika mpira eneo la hatari.
mwisho.
No comments:
Post a Comment