Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, May 6, 2016

YANGA KUWAKOSA KAMUSOKO NA NGOMA KESHO



YANGA kesho inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuivaa Sagrada Esperanca ya Angola, ikiwakosa wachezaji wake nyota raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Kamusoko na Ngoma ni msimu wao wa kwanza Yanga wakitokea FC Platinums ya  Zimbabwe,  ambapo Ngoma hadi sasa amecheza mechi 45 na kufunga mabao 24 na  Kamusoko amecheza mechi 46 na kufunga mabao tisa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ngoma mwenye mabao matatu aliyofunga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika alioneshwa kadi ya pili ya njano katika pambano la marudiano dhidi ya Al Ahly nchini Misri, ambapo kadi yake ya njano ya kwanza aliipata katika pambano la marudiano dhidi ya APR Uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
Kwa upande wa Kamusoko mwenye mabao mawili, alioneshwa kadi ya njano katika mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly pamoja na pambano la kwanza dhidi ya Cercle de Joachim.
Hata hivyo, kukosekana kwa wachezaji hao si pigo sana kwani kocha wa Yanga, Hans Pluijm ana hazina ya wachezaji ambao amekuwa akiwaanzisha katika mechi mbalimbali za ligi hiyo hivi karibuni, huku akiwaanzisha benchi Ngoma na Kamusoko.
Malimi Busungu ama Paul Nonga mmojawapo anaweza kuchukua nafasi ya Ngoma, huku ile ya Kamusoko akicheza  ama Salum Telela, Mbuyu Twite, Said Juma Makapu au Haruna Niyonzima.
Yanga imeangukia katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC),  baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria, Misri.
Yanga ilizitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani.
Katika Raundi ya kwanza waliitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa mabao 2-1, ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
Vingilio katika mchezo huo utakaochezeshwa  na waamuzi  kutoka Ghana, cha juu ni Sh 30,000 na chini ni Sh 5,000.
Akitangaza vingilio hivyo, Ofisa Uhusiano wa Yanga, Jerry Muro alisema vingilio vingine ni Sh 20,000  na Sh 7,000.
Pia alisema kukosekana kwa Ngoma na Kamusoko si tatizo na kwamba kocha ameshafanyia kazi suala hilo na mashabiki wasiwe na hofu, Yanga ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.
Kwa upande wake, Pluijm alisema amewapanga vyema vijana wake na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika mchezo huo.
“Tupo vizuri, tumejipanga kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wetu,” alisema Pluijm.

No comments:

Post a Comment