Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, May 6, 2016

STEWART KUONDOKA AZAM MWISHO WA MSIMU HUUAKIWA amedumu kwa muda wa siku 360, kocha Stewart Hall wa Azam sasa anahesabu siku kwa kuwa wiki mbili zijazo atafungasha kilicho chake na kupewa mkono wa kwa heri ndani ya klabu hiyo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Azam  na kuthibitishwa na Hall mwenyewe, ni kwamba kocha huyo ameandika barua ya kuachia ngazi ndani ya klabu hiyo, baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, huku akivurunda kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Chanzo hicho kilisema hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka pointi tatu Azam kwa kumchezesha Erasto Nyoni na hivyo kupoteza matumaini ya ubingwa pia kimechangia kocha huyo kujichuja.
 “Baada ya jana  (juzi) kukatwa pointi na kupoteza matumaini ya ubingwa, kilikaa kikao cha uongozi na Stewart Hall, moja ya masharti katika mkataba wake ulikuwa ni kuhakikisha Azam inatwaa ubingwa, na kuchukua Kombe la FA, pia kufanya vizuri michuano ya kimataifa.
“Kombe la Shirikisho tumetolewa, ubingwa ndo huo tumeshapoteza dira, ingawa bado tupo fainali ya Kombe la FA tukitarajiwa kucheza na Yanga, hivyo mwenyewe ameamua kujiondoa, “ kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wake Hall alipoulizwa jana alikiri kuwepo suala hilo la kuandika barua, lakini wamekubaliana ataendelea kuinoa timu hiyo hadi ligi itakapomalizika Mei 21 mwaka huu na fainali ya Kombe la FA.
 Alisema ameamua kujiondoa kwa sababu amegundua wachezaji hawamuelewi anachowaelekeza na haoni kama kuna maendeleo kadiri siku zinavyozidi kwenda.
Sababu nyingine iliyotajwa na kocha huyo raia wa England, ni pamoja na aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi chake kutokidhi matakwa yake, huku akidai haoni mustakabali wa baadaye ndani ya Azam.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa alipoulizwa jana kuhusu suala hilo hakuwa tayari kuzungumzia kwa maelezo hakuwa na jipya.
Katika kipindi alichoiongoza Azam, Hall ameshinda taji moja la Kombe la Kagame Julai 2015, lakini alishindwa kukiongoza kikosi chake kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho, ambalo walitolewa raundi ya pili na Esperance ya Tunisia.
Kocha huyo raia wa Uingereza, alianza kuinoa timu hiyo Mei 15 mwaka jana akichukua nafasi ya Mcameroon, Joseph Omong aliyefungashiwa virago, baada ya Azam kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika  na El Merreikh kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 na nafasi yake ikachukuliwa kwa muda na aliyekuwa kocha msaidizi, George ‘Best’ Nsimbe.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Hall kutimulia ndani ya klabu, awali alitimuliwa 2014, baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu msimu wa 2013/2014