Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa motisha kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanawake(Twiga Stars) ikishinda katika mchezo wake dhidi ya Zimbabwe unatarajiwa kuchezwa siku ya Ijumaa tarehe Machi, 4 katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Annastazia James Wambula alipotembelea kambi ya Timu hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wachezaji wa Twiga Stars, Wambura amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo wamekusanya shilingi milioni 15 ambazo zitatumika kama motisha kwa wachezaji hao.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa iwapo timu hiyo itaibuka na ushindi katika mechi yake dhidi ya Zimbabwe kila mchezaji atapata gawio la sh. Laki tatu kama motisha na kuongeza kuwa itafanyika hivyo hivyo katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Zimbabwe.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa michezo kuzidi kujitokeza na kuisaidi timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kwa wingi katika mechi ya tarehe Mach, 4 dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa katika uwanja wa Taifa.
Aliongeza kuwa msaada zaidi unahitajika ili kuiwezesha timu hiyo kukidhi mahitaji yake muhimu, hivyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kutoa michango yao kupitia Twiga Specila Fund, Akaunti na: 20110001677 iliyoko NMB tawi la Bank House jijjini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesiga ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha Twiga Stars inapata huduma muhimu ikiwemo motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Mwesiga pia amewapongeza wadau wote waliojitolea kusaidi timu hiyo ambapo amesema kujitokeza kwa wadau hao kunaongeza morali ya wachezaji.
Msaada huo wa shilingi milioni 15 umetolewa na wadau watatu ambapo mmja aliyechangia shilingi Milioni 3 aliomba jina lake lihifadhiwe, wengine ni Kampuni ya ASAS shilingi milioni 2 na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) sh. Milioni 10.
Wakati huohuo Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye amesema ili kuzidi kuwatia moyo wachezaji hao atawaongezea laki nne kwa kila mchezaji kama wataibuka na ushindi.
Mhe. Nnauye alisema hayo wakati akizungumza na kipindi cha E sport kinachorushwa na E fm na hivyo kupitia zawadi hiyo ya laki saba kwa kila mchezaji anaamini itaweza kuwapa motisha wachezaji ya kufanya vizuri katika kila mchezaji.
Na Frank Shijja
NW2Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Selestine Mwesiga akitoa shukura kwa Serikali kutokana na jitihada zake za kuitafutia wadhamini Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu wanawake (Twiga Stars) wakati Naibu Waziri wa Habari, Utamduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura(wapili kutoka kushoto) alipo watembelea wachezaji wa Timu hiyo leo jijini Dar es Salaam.Kutoka kulia ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a (kulia). Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Makoye Nkenyenge.
NW3Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura akisalimiana na Kocha wa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu wanawake “Twiga Stars” (Nasra Juma) alipowatembelea kambini kwao leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a.

NW5Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanawake “Twiga Stars” wakimsikiliza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura (hayupo pichani) alipowatembelea kambini kwao leo jijini Dar es Salaam.Twiga Stars inatarajiwa kucheza mechi na Timu ya Taifa wanawake ya Zimbabwe mchezo utakaochezwa tarehe 4 katika uwanjja wa Taifa. (Picha na Wizara ya Habari)