USHINDI wa mabao 5-0 iliyoupata leo dhidi ya Majimaji ya Songea umeiwezesha Yanga kurejea kileleni mwa msimamo
wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kutokana na ushindi huo wa jana
katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga imefikisha
pointi 39 sawa na Azam iliyochukua usukani juzi kutoka kwa Yanga, lakini uwiano
wa mabao ya kufunga na kufungwa unairudisha Yanga kileleni.
Azam ina mabao ya kufunga 30 na
imefungwa 10, wakati Yanga ina mabao ya kufunga 36 na imefungwa matano hivyo
kuwa na uwiano mzuri zaidi. Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33,
ambapo timu zote zimemaliza mechi 15 za duru la kwanza.
Katika mchezo wa jana, bao la
kwanza la Yanga lilifungwa dakika ya tano mfungaji akiwa Thabani Kamusoko
kutokana na pasi ya Deus Kaseke.
Majimaji walitulia kutaka
kusawazisha bao hilo na dakika ya 34 Marcelo Bonaventura alikosa nafasi ya
kufunga baada ya shuti lake kutoka pembeni kidogo ya lango la Yanga.
Majimaji iliendelea kufanya
mashambulizi ya kushtukiza, lakini umaliziaji haukuwa mzuri, hali ambayo pia
iliwakuta Yanga huku washambuliaji wake Amis Tambwe na Donald Ngoma wakishindwa
kutumia nafasi hizo kipindi cha kwanza.
Dakika ya 48 Yanga iliandika bao
la pili mfungaji akiwa Ngoma kutokana na pasi ya Kamusoko, wakati bao la tatu
lilifungwa dakika ya 56 na Tambwe.
Yanga iliendelea kulishambulia
lango la Majimaji ambayo ipo nafasi ya 14 katika timu 16 zinazoshiriki ligi
hiyo ikiwa na pointi 12, ambapo dakika ya 76 Tambwe alifunga bao la nne kutokana
na pasi ya Kaseke.
Tambwe aliifungia Yanga bao la
tano dakika ya 85, likiwa la tatu katika mchezo wa jana, lakini pia likiwa la
13 tangu msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara uanze na hivyo kuongoza katika
ufungaji akimuacha Hamisi Kiiza wa Simba mwenye mabao 10.
Naye Alexander Sanga anaripoti
kutoka Shinyanga kuwa Mwadui jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui, Shinyanga. Mabao ya Mwadui yalifungwa na
Jerry Tegete dakika ya 22 na Fabian Gwense dakika ya 51. Bao la Kagera
lilifungwa dakika ya 88 na Babu Ally.
No comments:
Post a Comment