Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (katikati) akimkabidhi jezi mmoja wa wawakilishi wa timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza ya StarTimes (SFDL) wakati wa hafla ya kukabidhi jezi hizo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano. Kushoto akipiga makofi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Malinzi. (Picha na mpiga picha wetu).
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (Kushoto) akimkabidhi jezi mmoja wa wawakilishi wa timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza ya StarTimes (SFDL) wakati wa hafla ya kukabidhi jezi hizo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu nchini, Bw. Boniface Wambura. (Picha na mpiga picha wetu)
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao (Kulia) akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jezi kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (SFDL) iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano. Katikati ni ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Malinzi na wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Selestine Mwesigwa.
(Picha na mpiga picha wetu).
Na Mwandishi Wetu.
KAMPUNI ya Urushaji wa Matangazo Kidijitali ya StarTimes ya Tanzania imekabidhi jezi kwa timu zinazocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Tanzania, ikiwa ni moja kati ya udhamini wa ligi hiyo ijulikanayo kama Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (SFDL).
Akizungumza na waandishi wakati wa kukabidhi jezi hizo jijini Dar es Salaam Jumatano, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa StarTimes Tanzania, Bw. Lanfang Liao alisema kuwa angependa kuona jezi hizo zinakuwa kama chachu ya kufanya vizuri kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu.
“Kwanza napenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ushirikiano huu wanaouonyesha kwetu kama StarTimes, lakini leo hii tunatoa jezi kwa timu za ligi hii ya daraja la kwanza ya StarTimes ikiwa ni sehemu ya udhamini wetu mbali na udhamini wa fedha za uendeshaji.”
“Jezi hizi sasa ni kama chachu ya timu zote za ligi daraja la kwanza kuongeza bidii na kufanya vizuri katika ligi hii msimu huu ili kuvutia wadhamini wengi zaidi. StarTimes kupitia udhamini huu tunaamini tumefungua njia kwa wengine nao kujitokeza na pia kuinua ari ya timu hizi,” alisema Bw. Liao.
Bw. Liao alisema kuwa kutokana na jitihada hizo angependa kuona wachezaji wanaocheza katika ligi hiyo wanacheza katika Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na timu nyingine kubwa kimataifa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Timu zinazoshiriki ligi hiyo, Bw Masao Bwire, aliipongeza kampuni ya StarTimes kwa kujitokeza kuipiga jeki ligi hiyo ambayo imekuwa ikiendeshwa bila udhamini wowote kwa kipindi kirefu.
Pamoja na hayo pia alilipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa jitihada zake za utafutaji wa wadhamini kwa lengo la kuinyanyua ligi daraja la kwanza nchini ambayo imekuwa ikizalisha wachezaji wanaocheza ligi kuu.
“Naipongeza kampuni ya StarTimes kwa kujitokeza kudhamini ligi daraja la kwanza. Hii ni hatua kubwa kwa ligi hii, kwa kuwa imekuwa ikienda bila udhamini kwa muda mrefu. Kukosekana kwa udhamini kulikuwa kukisababisha timu kutojiendesha vizuri hasa katika masuala ya vifaa, kulipa wachezaji na viongozi posho, kusafiri mbali kwa ajili ya mechi na usajili. Tunashukuru sana hayo sasa yatabakia historia na tunawaomba wadau wengine wajitokeze kwani bado hitaji ni kubwa. Lakini pia naipongeza TFF kwa jitihada zake kubwa za kutafuta wadhamini ili kusaidia maendeleo ya ligi hii nchini,” alisema Bw. Bwire.
Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Bw. Jamal Malinzi aliishukuru kampuni ya StarTimes kwa ushirikiano inaoutoa ili kuhakikisha ligi hiyo inasonga mbele na kuziasa timu zinazoshirki ligi hiyo kuongeza jitihada na kufanya vizuri baada ya kupata msukumo huo toka StarTimes.
“Napenda kuishukuru kampuni ya StarTimes kwa ushirikiano inaotuonyesha ili kuipeleka mbele ligi hii lakini pia naziasa timu zote zinazoshiriki ligi hii ya StarTimes ya Daraja la Kwanza kuongeza jitihada na kufanya vizuri katika msimu huu wa ligi. Pia ningependa kuwataka na nyinyi mfanye juhudi kutafuta wadhamini wengine kwani mnaweza kufanya hivyo ili kufanya ligi iwe na ushindani zaidi.” alihitimisha Bw. Malinzi.
No comments:
Post a Comment