TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars kesho itacheza na Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.
Kocha Mkuu wa Stars, Charles Mkwasa amesema kuwa Nigeria inafungika endapo
wachezaji wake watatimiza majukumu yao kama alivyowafundisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkwasa alisema anawashukuru watanzania kumuonesha ushirikiano na kuwaomba
kujitokeza kwa wingi leo.
Pia alisema mechi itakuwa nzuri, ikiwa kila mtu
atatekeleza majukumu yake, wanaweza kuibuka na ushindi kwa sababu hakuna timu
isiyofungika ila inategemea na wao wamejipangaje kuweza kushinda mchezo huo.
Mkwasa alibainisha mchezo utakuwa mgumu ila kwa
vile wamejiandaa tangu kambi ya Uturuki
watapambana mpaka mwisho kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwa hali na
mali ili kuwapa faraja watanzania.
Kukosekana kwa golikipa namba moja wa Nigeria,
Vincent Enyeama, Mkwasa alisema watatumia nafasi hiyo kuhakikisha wanafanya
mashambulizi lakini akasisitiza kuwa wao wamejipanga kuikabili Nigeria kama
timu na siyo mchezaji mmoja mmoja.
“Tutawakabili Nigeria kama timu na si mchezaji
mmoja mmoja, lakini kutokuwepo kwa kipa wao namba moja inaweza kuwa ni faida
kwetu japokuwa hata golikipa atakayedaka anaweza kuwa na kiwango cha juu
kumpita Enyeama lakini hapati nafasi kwenye timu,” alifafanua Mkwasa.
Mkwasa alisema safu ya ushambuliaji wamefanya
mazoezi ya kutosha juu ya kufunga wakiwa Uturuki na hata kwenye mazoezi baada
ya kurejea Tanzania, ana imani washambuliaji wake watafanya kile
alichokielekeza kwani timu ilicheza mechi tano bila kufunga hata bao moja
lakini tangu ameanza kuifundisha imefunga mabao mawili kwenye mechi mbili japo
haikupata ushindi.
Kwa upande wa kocha Sunday Oliseh, huu utakuwa
mtihani wake wa kwanza baada ya kurithi mikoba ya kocha Stephen Keshi
aliyeachia ngazi Julai.
Ingawa Stars iko nyuma ya Nigeria kwa nafasi 87
katika viwango vya ubora vya FIFA, bila shaka
itatoa changamoto kubwa dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika ambao
wameanza kuunda upya timu yao kupitia Oliseh.
Oliseh atakuwa akiangalia pia mchezo wa kundi
‘G’ kati ya Misri na Chad ambapo Misri wanaongoza kundi kwa tofauti ya mabao.
Mchezo huo utaanza saa 10:30 na utachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda ambao
ni Louis Hakizimana (kati), Honore Simba
(mwamuzi msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (mwamuzi msaidizi), Abdoul Karim
Twagiramukiza (mwamuzi wa akiba) na kamishna ni Charles Masembe kutoka nchini
Uganda.
Viingilio vya mchezo ni VIP A Sh 40,000, VIP B
Sh 30,000, VIP C Sh15,000, Rangi ya Machungwa (Orange) Sh 10,000, na viti vya
rangi ya Bluu na Kijani Sh 7,000.
No comments:
Post a Comment