MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro ( NCAA), imetoa Sh. 10, 486,000 kwa ajili ya kudhamini
tuzo za Wanamichezo Bora waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya uongozi wa
Rais Jakaya Kikwete.
Tuzo hizo zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA zinatarajiwa kufanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani
City, Dar es Salaam, ambapo pia TASWA itatoa Tuzo ya Heshima kwa Rais Kikwete
ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa sekta ya michezo katika uongozi wake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Adam Akyoo, alisema
wameamua kusaidiana na TASWA kwa sababu Rais Kikwete ni mdau mkubwa wa michezo
na pia wa masuala ya utalii.
‘’Dk. Kikwete ni mdau mkubwa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
kwani kwa kipindi chote ambacho amekuwa Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ametembelea
hifadhi hii mara nyingi zaidi kuliko viongozi wengine wote wa Taifa letu
waliomtangulia.
‘’Pia amekuwa mdau muhimu na wa mstari wa mbele wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro katika kutangaza vyema vivutio vya watalii vya hifadhi ya Ngorongoro
katika mataifa mbalimbali duniani alikokwenda kwa ziara za kikazi.
‘’Jambo hili limeleta watalii wengi nchini kutoka mataifa mbalimbali
dunini. Vile vile ziara zake za mapumziko hifadhini wakati wa sikukuu mbalimbali
zimewahamasisha sana Watanzania walio wengi kutembelea
hifadhi hii kutoka kote nchini na hata nchi jirani,’’ alisema Akyoo.
Pia alisema waandishi wa habari ni wadau wakubwa na muhimu katika
harakati za utalii na ndiyo sababu wameamua kuisaidia TASWA ifanikishe shughuli
yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliishukuru mamlaka
ya hifadhi hiyo na kusema kuwa msaada huo ni mkubwa na kuomba wadau wengine
waungane nao kufanikisha jambo hilo.
‘’Kama tulivyosema bajeti yetu ni Sh milioni 130, juzi (Jumatano)
tulipata watu wa GSM Foundation waliotupa Sh. Milioni 50, tunaomba na wengine
tushirikiane nao katika hili,’’ alisema Mhando.
Alisema
TASWA imeamua kuandaa hafla ya wanamichezo kumuaga Rais na pia kumpa tuzo kwa
vile wakati wa uongozi wake amefanya mambo makubwa katika sekta ya michezo.
Kwa
mujibu wa Mhando, wanamichezo pia watatumia tuzo hizo zilizoandaliwa na TASWA kumuaga
Rais Kikwete anayemaliza muda wake kikatiba baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani Oktoba 25, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment