TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars leo imerejea
nchini kutoka Misri ilipokwenda kucheza mechi ya kuwania kufuzu fainali za
Kombe la Mataifa Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita na kufungwa mabao 3-0.
Kwa muda mrefu Stars haijapata matokeo mazuri kwenye
mechi za kimataifa hali iliyofanya wachezaji wake kutoka uwanja wa ndege kwa
mafungu huku wengine wakikwepa kuzungumza na vyombo vya habari.
Timu hiyo iliwasili kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Julius Nyerere saa 7:30 mchana na wachezaji wake kuanza kutoka
mmoja mmoja wakiongozwa na Juma Abdul, kisha akafuata Salum Telela, Amri
Kiemba, Aggrey Moris na Jonas Mkude.
Tofauti na siku za nyuma, mashabiki hukusanyika
kuipokea timu hiyo pamoja na viongozi mbalimbali, leo hali ilikuwa tofauti
hakukuwa na kiongozi yeyote uwanjani hapo si kutoka Shirikisho la soka Tanzania
(TFF) wala kwa wadau wa soka.
Kila mchezaji alipotoka, madereva taxi wa uwanja wa
ndege walisema: “Eeh watalii mmerudi,
watalii mmerudi,”.
Akizungumza uwanjani hapo, mchezaji wa kimataifa anayecheza
TP Mazembe ya Congo DR, Mbwana Samatta alisema hakuna ubishi kwamba walicheza
na timu bora na kilichobaki ni kujipanga upya.
“Ni kweli mechi ilikuwa ngumu sana kama mlivyoona…
tulifungwa sababu muda mwingi tulikuwa tunazuia, sasa unategemea nini? si
unachoka,” alisema Samatta.
Naye nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub alisema
anajua watanzania wanaumizwa na matokeo hayo lakini wasikate tamaa, wanaahidi
watafanya vizuri kwenye mechi dhidi ya Uganda Jumamosi ( Kuwania kufuzu fainali
za mataifa kwa wachezaji wa ndani, CHAN)
ili kurudisha imani.
No comments:
Post a Comment