UONGOZI wa Yanga umemtambulisha rasmi mchezaji wake mpya Deus Kaseke na kumkabidhi rasmi jezi namba nne iliyokuwa ikivaliwa na Rajab Zahir ambaye mkataba wake umekwisha. Kaseke alisajiliwa juzi kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea Mbeya City alikotumika kwa miaka minne na mkataba wake umemalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu
wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro, Zahir mkataba wake
umekwisha hivyo wanaendelea na mazungumzo naye na wakati wowote wataweka wazi
kama watamsajili au aende zake. Muro alisema Kaseke alikuwa ni bora ndio maana
walivutiwa na kipaji chake wakiamini anaweza kuisaidia timu kufanya vizuri msimu
ujao.
“Ni furaha
kubwa kuwa na mchezaji mwenye kipaji kikubwa tunaamini atatusaidia Yanga kufanya
vizuri, ni mchezaji mzuri amekuja kucheza katika timu ya kimataifa na atakuwa
wa kimataifa,” alisema.
Alisema
mchezaji huyo ni mzalendo na ameonesha uwezo mkubwa msimu uliopita ndio maana
wamevutiwa naye.
Kwa upande
wake, Kaseke alisema amefuhi kupata nafasi ya kuitumikia klabu hiyo na kuahidi kuendelea
kuonesha juhudi pale alipoachia na kuiwezesha Yanga kufanya vizuri.
“Nawashukuru
Mbeya City hadi mkataba wangu ulipoisha tulifanya kazi vizuri, lakini pia
nafurahia sehemu nilipo sasa kwani ndoto yangu imetimia nilitamani kucheza michezo
ya kimataifa,”alisema.
Kaseke
ambaye amezaliwa miaka 21 iliyopita, ana uwezo wa kucheza namba saba, 11 na 10
na amesajiliwa na timu hiyo ili kuziba nafasi iliyoachwa na Mrisho Ngassa aliyesajiliwa
na Free State Stars.
Alisema
atapambana kwa uwezo wake kuonesha juhudi ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza
na kufanya vizuri zaidi katika michezo ya kimataifa.
Muro alisema
wachezaji wengine wataendelea kusajiliwa siku za karibuni na kutambulishwa,
hivyo kuondoa uvumi kuwa wamemsajili mchezaji fulani.
Miongoni mwa
wachezaji wanaopewa nafasi ya kusajiliwa na Yanga ni Haruna Chanongo, ambaye
mkataba wake umemalizika Simba.
Pia,
alitangaza rasmi kuwasajili kwa mara nyingine kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima
kwa mkataba wa miaka miwili, Mbuyu Twite mwaka mmoja na Deogratias Munishi
miaka miwili.
No comments:
Post a Comment