SIMBA leo imeendeleza ubabe dhidi ya Yanga katika mchezo wa
Kampeni ya Nani Mtani Jembe baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika
mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo kama huo Desemba 21 mwaka jana Simba iliibuka na
ushindi wa mabao 3-1, yaliyofungwa na Amis Tambwe na Awadh Juma.
Mchezo huo ulichezeshwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa, ikiwa ni
mara ya kwanza katika historia mechi ya Simba na Yanga mwanamke kupuliza filimbi.
Mfungaji wa bao la tatu katika mchezo kama huo mwaka jana,
Awadhi Juma, ndiye jana alifunga bao la kwanza dakika ya 30 akimalizia mpira wa
adhabu uliopigwa na Emmanuel Okwi na kutemwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya sana wachezaji wa Yanga
na kujikuta wakicheza hovyo, hali iliyosababisha wafungwe bao la pili dakika ya
40, mfungaji akiwa Elius Maguli.
Maguri alifunga bao hilo baada ya mpira wa kichwa aliopiga
kugonga nguzo ya goli na kurejea uwanjani na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha
wavuni na kumuacha Dida akigaagaa.
Yanga ingeweza kupata bao la mapema kutokana na kufanya
mashambulizi ya kushtukiza baada ya kuanza mchezo huo, lakini umalizijia
haukuwa mzuri.
Mshambuliaji mpya wa Yanga, raia wa Liberia, Kpah Sherman
mara kadhaa alijaribu kufurukuta lakini alikosa ushirikiano wa kutosha.
Simba nayo licha ya ushindi huo, lakini washambuliaji wake
wakiongozwa na Simon Sserunkuma, Elias Maguli na Emmanuel Okwi walipata nafasi
za kufunga, lakini walishikwa na kigugumizi cha miguu kila waliposogea eneo la
hatari.
Kipindi cha pili, Yanga ilipata pigo baada ya Sherman
kuumia, hivyo kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Mrisho Ngassa.
Dakika ya 62, Danny Mrwanda aliyeingia kipindi cha pili
badala ya Andrey Coutinho nusura aipatie Yanga bao, baada ya mpira aliopiga
kuokolewa na beki Hassan Isihaka, wakati kipa Ivo Mapunda hayupo golini.
Dakika ya 67 Sserunkuma akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga,
shuti lake lilipaa juu kidogo ya lango la Yanga, huku tayari baadhi ya
mashabiki wa Simba wakianza kuinuka wakiamini amefunga.
Simba: Ivo Mapunda, Nassor Masoud, Mohammed Hussein/Issa
Rashid,
Hassan Isihaka, Juuko
Murishid/Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Said Ndemla, Awadh Juma,
Elius Maguri/Danny Sserunkuma, Simon Sserunkuma/Shaaban Kisiga na Emmanuel
Okwi.
Yanga: Deogratius Munishi, Abdul Juma/Hussein Javu,Oscar
Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite/Hassan Dilunga, Haruna
Niyonzima, Emerson Roque/Salum Telela, Simon Msuva, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa
na Andrey Coutinho/Danny Mrwanda.
No comments:
Post a Comment