Mechi ya
Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager itachezwa Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George
Kavishe amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi
ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match). Pambano hili ni zawadi ya
kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba
itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe
aliongeza kuwa mechi hii ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani
Mtani Jembe 2 ambayo imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa
mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya
Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2 inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na
Yanga ambapo zawadi ya shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
- Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
- Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema
mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa kununua bia ya Kilimanjaro
Premium Lager yenye ujazo
wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro
Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au
YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma kwenda namba 15415
na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa taslimu shilingi 10,000 kutoka
timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia
alizikabidhi timu hizo jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi
hiyo na kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa kuhakikisha
wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo lazima mshindi
apatikane.
Mkurugenzi
wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura
aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu
hizo ziko kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa
kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja
viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C,
15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku
viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura
alisema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa
kwa dakika 90 tu ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya
penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la Nani
Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika
mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.
No comments:
Post a Comment