YANGA SC
imesema itatuma majina ya wachezaji sita wa kigeni katika usajili wao kwa ajili
ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, badala ya watano wanaotakiwa kwa mujibu
wa kanuni.
Mwenyekiti
wa Yanga SC, Yussuf Manji amewaambia Waandishi wa Habari leo makao makuu ya
klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani kwamba, jina la mshambuliaji
Emmanuel Okwi kutoka Uganda litaongoza orodha hiyo.
Mbali na
Okwi, wachezaji wengine wa kigeni wa Yanga SC ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima
kutoka Rwanda, Mganda Hamisi Kiiza na Wabrazil, Andrey Coutinho na Geilson
Santana ‘Jaja’.
Lakini Okwi,
pia amesajiliwa na Simba SC, maana yake usajili ya Mganda huyo utazua tafrani
mbele ya safari.
Dirisha la usajili kwa wachezaji wazalendo linatarajiwa kufungwa leo, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongea siku mbili zaidi tangu juzi.
Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kwamba, sababu za kusogeza mbele ni klabu zote za Ligi Kuu kushindwa kukamilisha usajili juzi.
“Nadhani wameshindwa kutumia huu mfumo wetu mpya wa elektroniki, sasa tumewapa Saa 48 zaidi warekebishe, zikiisha hapo hakuna nafasi tena, tunasonga mbele,”amesema Mwesigwa.
Amesema kwamba hadi muda wa kufunga usajili juzi Saa 6:00 usiku, ni timu moja tu, Kimondo FC ya Daraja la Kwanza ndiyo iliyokuwa imefanikiwa kukamilisha usajili wake katika mfumo huo. “Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Kimondo kwa kumudu kuutumia mfumo huu na kuwasilisha usajili wao ndani ya muda,”amesema.
Aidha, Mwesigwa amesema kwamba dirisha la usajili kwa wachezaji wa kigeni litafungwa Septemba 6, mwaka huu. “Hili dirisha la wachezaji wa kigeni likifungwa, hakuna nyongeza ya muda tena, kwa kuwa hili lipo katika mfumo wa kimataifa chini ya FIFA, likifungwa, limefungwa dunia nzima, hivyo nawasihi viongozi wa klabu wahakikishe hawafanyi makosa,”amesema.
No comments:
Post a Comment