Meneja wa Arsenal Arsen Wenger |
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amekiri kwamba
anadhamiria kuwaita wachezaji wake wa Ujerumani walioshinda Kombe la
Dunia warudi kwenye kikosi mapema kwa ajili ya mechi ya kwanza ya kufuzu
kwa makundi katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne ugenini Besiktas.
Gunners wataenda Uturuki baada ya kutolewa jasho mechi yao ya kwanza
Ligi ya Premia nyumbani dhidi ya Crystal Palace ambao hawakuwa na
meneja, na ambapo waliokolewa na bao la dakika za mwisho kutoka kwa
Aaron Ramsey lililowawezesha kushinda 2-1 dhidi ya vijana 10 wa palace.
Wenger alikuwa amewapa Wajerumani wake Mesut Ozil, Per Mertesacker na
Lukas Podolski muda zaidi wa kupumzika baada ya taifa lao kushinda
Kombe la Dunia Brazil mwezi jana.
Lakini baada ya Kieran Gibbs kupata jeraha la misuli ya paja
akicheza dhidi ya Palace na Jack Wilshere pia kuondolewa mapema baada ya
kugongwa, Mfaransa huyo alikiri kwamba anashawishika sana kuwaita
Wajerumani hao.
“Mechi hiyo ya kfuuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni kubwa sana
kwetu dhidi ya Besiktas, tuna muda mfupi sana wa kumpumzika,” akasema
Wenger.
"Kawaida, wachezaji hao wa Ujerumani hawangecheza mechi hiyo. Tutaangalia Jumapili lakini ni kukiwa na dharura pekee.
"Kwa sababu ya Crystal Palace kutumia nguvu na mpangilio wao pia
ilikuwa vigumu sana kwetu.
Tulifungwa bao kutoka na kona ya kwanza kwa
sababu bado tunapungukiwa na kasi thuluthi ya mwisho tunapopanga
mashambulizi maeneo hatari.
"Lakini tuliendelea kupambana na hilo lilitosha kushinda mechi hiyo.
Siku ya kwanza ya mechi, sisi ndio pekee tulishinda nyumbani na kwa
hivyo hilo linaonyesha ugumu uliokuwepo kwa kila mtu siku ya kwanza.
Tulipata alama tatu tulizotaka, sasa hebu tuangazie Besiktas."
Mchezaji aliyenunuliwa majuzi Alexis Sanchez alihangaika mechi yake
ya kwanza Ligi ya Premia dhidi ya Palace waliotumia nguvu sana.
Fowadi huyo wa Chile, aliyewagharimu £30milioni kutoka Barcelona, alionekana kama mchezaji anayezoea mazingira yake mapya.
“Nina furaha sana na mtazamo wake kwa sababu aliendelea kupigana
dakika zote 90, hata ingawa hayuko sawa kabisa kimwili,” akasema Wenger.
"Kiufundi, anahitaji kuimarisha ufahamu wake wa washirika wake na alionekana mwenye kuchangamka na hatari hadi mwisho.”
No comments:
Post a Comment