Kocha wa timu ya taifa ya Argentina Alejandro Sabella katikati akifurahia ushindi wa penati dhidi ya Uholanzi katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la dunia nchini Brazil uliopigwa jana |
Siku moja baada ya kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua
ya fainali, kocha wa timu ya taifa ya Argentina Alejandro Sabella, ametangaza
kulipa kisasi dhidi ya timu ya taifa ya Ujerumani kwa niaba ya mataifa ya
Amerika ya kusini yaliyoshiriki michuano ya kombe la dunia ya mwaka huu, huko
nchini Brazil.
Sabella, ametangaza hali hiyo huku akitambua fika mashabiki
wa soka wa ukanda wa Amerika ya kusini, watakua wanaiunga mkono timu yake
ambayo itakua na shughuli ya kupambana na taifa kutoka barani Ulaya (Ujerumani).
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 amesema kikosi chake
kipo tayari kupambana hadi tone la mwisho la jasho, kwa ajili ya kuhakikisha
ubingwa unabaki kwenye ardhi ya bara la Amerika ya kusini.
Hata hivyo amesema mpango alioutangaza haumaanishi kama anawabeza
wapinzani wao Ujerumani, bali anawaheshimu kutokana na mchezo mzuri wa soka
walio uonyesha tangu alipoanza mshike mshike wa kushiriki fainali za kombe la
dunia za mwaka huu.
Kauli ya Alejandro Sabella, huenda ikawapa faraja mashabiki
wa soka wa nchini Brazil ambao bado wanakumbuka kichapo cha kadhia cha kufungwa
mabao saba kwa moja kilichowaangukia siku mbili zilizopita kutoka kwa
Ujerumani.
Mchezo wa kumsaka bingwa wa fainali za mwaka 2014,
utachezwa siku ya jumapili katika uwanja wa Maracana uliopo mjini Rio de
Janeiro, ukitanguliwa na mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu utakaochezwa siku ya
jumamosi kwenye uwanja wa Nacional Mané Garrincha, mjini Brasília kati ya
wenyeji Brazil dhidi ya Uholanzi.
No comments:
Post a Comment