TIMU ya
Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ itaondoka kesho kuelekea
nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kufunzu kombe la dunia
huku ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri.
Katika mechi
ya kwanza dhidi ya Afrika Kusini iliyochezwa hivi karibuni kwenye uwanja wa
nyumbani wa Taifa wa Dar es Salaam, Tanzanite ilichapwa mabao 4-1, hivyo
inahitaji kushinda katika mchezo huo kuanzia mabao 5 ili iweze kusonga mbele.
Kaimu Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) Boniface Wambura alisema jana kuwa
timu hiyo wakiongoza na kiongozi mmoja wa msafara wataondoka kuanzia saa nne na
nusu kwa ndege ya Fast Jet.
Akizungumzia
maandalizi ya mchezo huo wa marudiano Kocha wa Tanzanite Rogasian Kaijage
alisema wana matumaini ya kufanya vizuri kwa vile walirekebisha mapungufu
yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza dhidi ya timu hiyo.
“Mchezo
uliopita ulikuwa na mapungufu kidogo,
lakini kwa sasa tumeshayarekebisha na tuna imani ya kufanya vizuri jambo la
muhimu ni watanzania kutuombea,”alisema.
Kaijage
alisema licha ya kufanya vibaya katika mechi ya kwanza wanahitaji kupewa moyo
na sio kulaumiwa kwa kupoteza mchezo mmoja, kwa vile huweza kuwakatisha tamaa
wachezaji.
Kwa upande
wake, Nahodha wa timu hiyo Fatma Issa aliomba watanzania kuacha kuwakatisha
tamaa na badala yake wawape moyo na kuwaombea ili kurudi na ushindi.
Alisema
“tunaahidi kufanya vizuri kwasababu tayari Kocha amerekebisha mapungufu, jambo
la muhimu nawaomba watuombee,”.
Aliwataka
watanzania kutovunjika moyo kwa matokeo mabaya yaliyopita na kuongeza kuwa
kutokana na marekebisho makubwa yaliyofanywa wana imani ya kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment