Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, December 13, 2013

KENYA MABINGWA WA CHALENJI 2013

Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
KENYA ‘Harambee Stars’ ndiyo mabingwa wapya wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya usiku huu kuifunga Sudan ‘Mwewe wa Jangwani’ mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Shukrani kwake, Nahodha wa timu hiyo, Alan Wanga aliyefunga mabao yote hayo katika mchezo wa leo uliokwenda sambamba na sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Kenya.


Wanga alifunga bao la kwanza dakika ya 35 kwa kichwa akiunganisha krosi ya David Ochieng Owino kutoka kushoto na la pili dakika ya 69 akiunganisha kwa guu la kulia krosi ya chini ya James Situma kutoka kulia pia.
Hilo linakuwa taji la sita la Challenge kwa Kenya, baada ya awali kutwaa katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002.
Mchezo huo, ulichelewa kuanza kutoka Saa 10:00 jioni hadi Saa 12:00 jioni kutokana na Sudan kuzuiliwa kutoka hotelini kwa sababu, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) halijawalipia gharama za malazi.
Ikabidi Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye aingilie kati hadi timu hiyo ikaruhusiwa kwenda Nyayo.
Awali, katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Zambia ‘Chipolopolo’ iliifunga Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Kipa Ivo Mapunda alipangua penalti mbili za Wazambia, Justin Zulu na Kondwani Mtonga, lakini Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa na Nahodha Kevin Yondan wote wakakosa penalti zao zikiokolewa na kipa wa Chipolopolo, Joshua Titima.
Waliofunga penalti za Zambia ni Felix Katongo, Ronald Kampamba, Bronson Chama, Julius Situmbeko, Rodrick Kabwe na Kabaso Chongo, wakati za Stars zilifungwa na Mbwana Samatta, Erasto Nyoni, Himid Mao, Amri Kiemba na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Katika mchezo huo, Zambia walitangulia kupata bao dakika ya 52 kupitia kwa Ronald Kampamba kabla ya Mbwana Samatta kufunga bao zuri mno dakika ya 65 akiisawazishia Stars.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika sita, kuanzia dakika ya 88 kufuatia Polisi kufyatua mabomu ya machozi wakipambana na mashabiki wa Kenya waliokuwa wanataka kuingia bure uwanjani.
Wachezaji walianza kuanguka mmoja mmoja kutokana na kuzidiwa na hewa ya mabomu, hivyo marefa wakasimamisha mchezo kabla ya kuanza tena dakika sita baadaye. 
Kwa matokeo hayo, Stars inaondoka Challenge ya 2013 na nafasi ya nne kama mwaka jana mjini Kampala, Uganda ilipofungwa kwa penalti pia na Zanzibar katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.
Kwa kutwaa ubingwa, Harambee walikabidhiwa hundi ya ya dola za Kimarekani 30,000 na rais wa CECAFA, Leodegar Tenga, wakati washindi wa pili, Sudan walipewa hundi ya dola 20,000 na washindi wa tatu, Zambia dola 10,000.

No comments:

Post a Comment