MGOMBEA wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Athman Nyamlani ametaja vipaumbele tisa vya maendeleo ya soka, iwapo atapata
ridhaa ya wapiga kura kuliongoza Shirikisho hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO), ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi utakaofanyika
Jumapili, Nyamlani alisema akipewa nafasi hiyo, atainua kiwango cha soka kwa kuimarisha usimamizi wa menejimenti ya
soka katika ngazi zote.
Nyamlani ambaye ni Makamu wa
Rais anayemaliza muda wake alisema endapo atapata ridhaa ya wapiga kura
kuliongoza shirikisho hilo pia atahakikisha
kunakuwepo na mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi na kusimamia sheria na
taratibu za uendeshaji wa soka la Tanzania na suala la viongozi kujiendeleza kielimu litapewa kipaumbele na
litakuwa ni agenda endelevu.
Alisema kuwa kama atakuchagulia pia
atapambana na vitendo vya rushwa katika soka kwa kuwa vimekuwa kikwazo kikubwa
katika upatikanaji wa maendeleo endelevu ya mchezo huo.
“Naomba nikiri kuwa kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa
ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka, wachezaji, waamuzi na wadau wengine.
Hivyo basi kwa kushirikiana na serikali na viongozi wa soka katika ngazi zote
nitahakikisha naendeleza mapambano dhidi ya rushwa katika mchezo soka, kuanzia
katika ngazi za uongozi na soka la viwanjani,” alisema.
Alisema kipaumbele cha tatu kitakuwa ni kukuza soka la watoto,
vijana na wanawake, na kwamba akiwa kama
Rais wa TFF, atalipa uzito wa kipekee soka la watoto wenye umri wa miaka chini
ya 16 na soka la vijana na kukuza vipaji kuanzia miaka tisa hadi 21 na soka ya
wanawake.
Nyamlani alisema kazi hiyo ataitekeleza kwa kuanzisha program mbali
za mashindano na za kukuza vipaji kwa makundi haya ya vijana kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wa soka.
“Katika uongozi unaomaliza muda wake tumejitahidi sana
kuyasukuma makundi haya na yameonyesha mwanga, hivyo nikishika wadhifa kama Rais nitaendeleza programu hizi kwa kushirikiana na viongozi wa soka katika ngazi
mbalimbali na serikali,” alisema.
Kipumbele kingine muhimu ni Kuimarisha Uwezo wa Rasilimali Fedha wa
Shirikisho, kama Rais wa TFF atahakikisha kuwa
TFF inapata vyanzo endelevu na vya kuaminika ili kuweza kujenga uwezo wa
shirikisho katika kutekeleza mipango kikamilifu.
No comments:
Post a Comment