Kamati
ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio
(revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya
Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20
kujihusisha na mpira wa miguu.
Sekretarieti
ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili
ili kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa
Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.
Uamuzi
huo wa mapitio umesomwa Oktoba 15 mwaka huu mbele ya
waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu
Mwenyekiti Victoria Makani.
Rukambura
amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika
mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu
cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu yake
itamalizika Oktoba 15, 2033.
Kabla
ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni
mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba
ya Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’
kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Pia
imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya
TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za
kawaida, na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo
(judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani
mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye
Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni
Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na
klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani
ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni
‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii
za TFF toleo la 2013.
Hivyo
Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi
ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Kamati
ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja
anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo
atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha
6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius
Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha
73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa
ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba
uongozi TFF.
Hivyo,
amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya
RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti
ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo
wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha Makocha
wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha fomu
yake ya kugombea.
Naye
Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya
Utendaji bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa
mujibu wa Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.
Amepigwa
faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo
akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza
kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile
Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa
Kamati ya Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo
vyao.
Pia
Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga
Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF
toleo la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu
ya kinidhamu inayomalizika 2014.
Hivyo,
amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na
ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF,
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa
Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa
kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati akitumikia
adhabu ya kufungiwa.
Kamati
ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili
kama ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala na
Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata
Katiba na Kanuni za TFF.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013,
uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa ya rufani wala
marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na Mahakama ya
Usuluhishi wa Michezo (CAS).
TFF YATOA KITANDA CHA UPASUAJI HOSPITALI YA TEMEKE
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekabidhi kitanda cha upasuaji kwa
Hospitali ya Rufani ya Manispaa ya Temeke, ikiwa ni sehemu ya mchango
wake kwa jamii.
Makabidhiano
hayo yamefanyika Oktoba 15 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa
TFF ambapo Hospitali ya Temeke iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya
hospitali hiyo James Syaga, Mganga Mkuu Dk. Amaani Malima na Matroni wa
hospitali hiyo Deodata Msoma.
Akikabidhi
kitanda hicho chenye thamani ya sh. milioni 6.8, Katibu Mkuu wa TFF,
Angetile Osiah alisema amefurahi kuwa ahadi ya kukabidhi msaada huo wa
Hospitali ya Temeke umetimia licha ya kuchukua muda mrefu kutokana na
ukweli kuwa fedha za kununulia kitanda hicho zinatokana na mchezo wa
Ngao ya Jamii wa mwaka jana kati ya Simba na Azam FC.
Alisema
uamuzi wa kuiteua Hospitali ya Temeke ulitokana na ukweli kuwa pamoja
na kwamba ofisi za TFF ziko wilayani Ilala, shughuli nyingi kubwa za
Shirikisho linafanyika kwenye Manispaa ya Temeke na hivyo hospitali hiyo
hufanya kazi kubwa ya kuhudumia watu mbalimbali wanaopata matatizo
wakati wa michezo ya mpira wa miguu.
Naye
Mganga Mkuu wa Hospitali, Dk. Malima aliishukuru TFF kwa kutimiza ahadi
yao na kwamba msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa wana vyumba
vitatu vya upasuaji, lakini ni viwili tu vilivyo na vitanda kwa hiyo
kitanda hicho kitakamilisha chumba hicho kianze kufanya kazi.
Alisema
Hospitali yake sio tu inahudumia wagonjwa kutoka wilayani Temeke, bali
kutoka hata Mkoa wa Mtwara na sehemu nyingine zinazozunguka wilaya hiyo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Hospitali, James Syaga, ambaye alisema anawakilisha watu
wanaohudumiwa na Hospitali ya Temeke, alishukuru kwa msaada huo na
kuiomba TFF kuendelea kuangalia uwezekano wa kusaidia hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment