Wednesday, October 23, 2013
ALICHOBWATUKA SIR ALEX FERGUSON KWENYE KITABU CHAKE
MANCHESTER, England
KILE kitabu cha maisha ya Sir Alex Ferguson, kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kimezinduliwa juzi, Manchester, England.
Ndani ya kitabu hicho, Ferguson amefunguka kuhusu ishu kibao ambazo ziliwahi kutawala vichwa vya habari enzi za utawala wake, Manchester United ambao ulidumu kwa miaka 27.
Kwenye kitabu hicho, Fergie amebwabwaja kuhusu ishu zake na David Beckham, Steven Gerrard, Paul Scholes, Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na namna alivyopata auheni Roy Keane alipoondoka Old Trafford mwaka 2005.
Hivi ni baadhi ya vitu muhimu kwenye kitabu hicho cha Ferguson.
ISHU YA WAYNE ROONEY
Ferguson amethibitisha kwamba, Wayne Rooney alitaka kuondoka Man United, mwisho wa msimu uliopita, huku akitoboa kwamba wakala wake, Paul Stretford ndiye aliyeshikia bango suala hilo.
Fergie pia amefunguka ni jinsi gani Rooney alihangaika kubaki kwenye kiwango cha juu tofauti na wachezaji kama kina Ryan Giggs na Ronaldo.
Kuhusu ishu ya Rooney kutaka kuhama ambayo mwenyewe amekuwa akiikanusha, Fergie ameandika: “Alikuja (Rooney) ofisini kwangu siku moja baada ya kushinda ligi na kuomba kuondoka.
“Hakuwa na furaha kutokana na kuwekwa benchi kwenye baadhi ya mechi. Wakala wake, Paul Stretford alimpigia simu David Gill na kusisitiza kuondoka.”
KUHUSU STEVEN GERRARD
Ferguson anaamini Steven Gerrard siyo kiungo bora sana na alikuwa akifunikwa katikati ya uwanja na Roy Keane na Paul Scholes.
Lakini Ferguson amekiri kwamba aliwahi kutaka kumsajili nahodha huyo wa Liverpool mwaka 2005, baada ya kusikia kuwa siku zake Anfield zinahesabika.
Ferguson anadai kwamba alikuwa akishangazwa na namna Gerrard alivyokuwa akitumika chini ya Rafael Benitez, anahoji kwanini hakupangwa kati, badala yake alipelekwa pembeni, yeye anaamini Gerrard ndiye alikuwa kiungo pekee ambaye alikuwa anaweza kuwaumiza akicheza katikati.
Alihitimisha kwa kudai kwamba, Gerrard alikuwa na uwezo wa kuibeba timu mwenyewe, lakini anaamini amefanikiwa zaidi katika timu ya taifa kuliko klabu.
ISHU YA DAVID BECKHAM
David Beckham alichagua usupastaa badala ya kutimiza uwezo wake na kuwa gwiji United, ameandika Ferguson.
Akizungumzia kuondoka kwa Beckham, Old Trafford, Ferguson amegoma kuomba radhi kuhusu kiatu cha uso alichompiga, badala yake amedai kwamba, Beckham alijiona ni zaidi yake.
Ferguson alieleza jinsi alivyomtwanga Beckham kiatu cha uso, anadai kwamba timbwili lilisababishwa na kitendo cha Beckham kushindwa kumkaba Sylvain Wiltord wakati wa mechi ya Kombe la FA, ambayo United ilipigwa 2-0 na Arsenal, Februari 2003 na kusababisha bao la pili.
Ferguson amesema: “Ndio alisimama kujibishana na mimi na wachezaji wengine walimzuia wakimwambia kaa chini, nikamwambia umeiangusha timu.” Baada ya hapo kiatu cha uso kikafuata.
ISHU YA ROY KEANE
Ferguson anadai kwamba, tabia za Roy Keane zilianza kubadilika alipoanza kupoteza utawala wake katikati ya uwanja na alipoanza kuhoji uwezo wa Fergie, kocha huyo amefunguka kila kitu juu ya kuondoka kwa Keane Old Trafford.
Fergie anadai kwamba, alipumua baada ya Keane kuondoka mwaka 2005, kwa sababu jamaa huyo alikuwa mropokaji sana.
Anadai kwamba, Keane alikuwa na sauti sana kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya United na siku akiwa na hasira hali itakuwa tete ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.
KUHUSU CRISTIANO RONALDO
Ferguson amemuelezea Ronaldo kama mmoja wa wachezaji bora aliowahi kufanya nao kazi na amemmwagia sifa Wayne Rooney kwa kumshawishi Ronaldo abaki Old Trafford baada ya England kutolewa robo fainali ya Kombe la Dunia na Ureno mwaka 2006.
Ronaldo aliibuka kuwa adui namba 1 wa England, kutokana na kumsababishia Rooney kadi nyekundu alipomkanyaga Ricardo Carvalho.
Ronaldo alitaka kuondoka England, lakini Fergie anadai kwamba Rooney ndiye aliyemshawishi abaki.
Rooney alimpigia simu Ronaldo na kumwambia hana bifu naye baada ya kadi nyekundu na kumwambia Fergie aandae mahojiano na waandishi wa habari ili waonyeshe umoja wao.
KUHUSU LIVERPOOL
Ferguson ameishambulia Liverpool kwa kudai kwamba inahitaji wachezaji nane zaidi kushinda taji la ligi, huku pia akimponda adui yake Rafa Benitez.
Fergie amemuita Benitez mpumbavu kwenye kitabu chake, huku akidai kwamba jamaa hana rafiki.
Pia ameiponda Liverpool kama klabu kwa jinsi ilivyolichukulia suala la Luis Suarez na uteuzi wa Brendan Rodgers. Fergie amedai kwamba, Michael Owen alikuwa mchezaji bora akiwa United, kuliko Liverpool.
Hakuishia hapo ameponda usajili uliofanywa na Kenny Dalglish kwa Stewart Downing, Jordan Henderson na Andy Carroll. Lakini mtu aliyemponda sana ni Benitez.
KAZI YA ENGLAND
Ferguson ametoboa kwamba, FA imewahi kumfuata mara mbili kwa nia ya kutaka kumpa timu ya taifa ya England, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1999, kabla ya uteuzi wa Kevin Keegan na mara ya pili ilikuwa mwaka 2001 kabla ya uteuzi wa Sven Goran-Eriksson.
FA iliwahi kumuomba kutokuzungumza ishu za Harry Redknapp kupewa majukumu ya kumrithi, Fabio Capello, kabla ya kumpa timu Roy Hodgson.
KUHUSU RIO FERDINAND
Ferguson amewaangushia lawama wapimaji dawa zilizopigwa marufuku michezoni kwa kumruhusu, Rio Ferdinand kuondoka uwanja wa mazoezi wa Manchester United na kukosa vipimo kisha kumfungia miezi nane mwaka 2003.
Ferguson anadai aliwahi kumuonya Ferdinand kuachana na mambo ya nje ya uwanja na kuelekeza akili yake uwanjani, kutokana na beki huyo kutaka kumuhoji rapa P Diddy.
“Usinichanganye Rio (Ferdinand), atakusaidia (P Diddy) kukufanya uwe beki bora.” Alisema Fergie, ambaye anadai kwamba ni shabiki mkubwa wa beki huyo.
@@@@@
Mashimo mbio za ubingwa England
LONDON, England
LIGI Kuu England inazidi kushika kasi, kila mechi ni kama fainali, timu ndogo hazikubali kushindwa timu kubwa zinataka kujikusanyia pointi zao mapema.
Ni mapema mno kuanza kutabiri bingwa, lakini kwa mechi kadhaa zilizochezwa mpaka sana, unaweza kuchanganua udhaifu wa kila timu.
Arsenal, Chelsea, Manchester City, Liverpool, Tottenham Hotspur na Manchester United ndio zinapewa nafasi ya ubingwa na makala haya yanaangalia udhaifu unaotakiwa kufanyiwa kazi katika kila timu.
Arsenal
Wamekosa mastraika
Jenkinson bado hajakomaa
Arsenal wameanza msimu kwa kasi ya ajabu, ujio wa Mesut Ozil umeboresha kikosi cha Arsene Wenger kinachoongoza Ligi Kuu England.
Ukubwa wa kikosi cha Wenger unatia hofu na anaweza kupata tabu katikati ya msimu, anahitaji kuongeza nguvu Januari. Arsenal inaviungo wengi ila mbele ni tatizo.
Olivier Giroud ndiye mchezaji muhimu kuliko wote kwenye kikosi kwa sasa, kwa sababu hakuna mbadala wake sahihi. Nicklas Bendtner, Chuba Akpom na Yaya Sanogo hawana hadhi ya kuongoza mashambulizi ya Arsenal, Lukas Podolski au Theo Walcott siyo washambuliaji kamili.
Tatizo jingine kwa Wenger ni beki ya kulia, Bacary Sagna anatajwa kuondoka na Carl Jenkinson bado sana kukomaa. Hili ni eneo jingine wanatakiwa kuimarisha Januari.
Liverpool
Viungo hawafungi
Hakuna mbadala wa Lucas na Gerrard
Kama Arsenal, Liverpool nao wameanza na moto msimu huu, hawana dalili za kuchukua ubingwa, lakini wanaweza kurudi nne bora mwisho wa msimu.
Brendan Rodgers anaonekana kupata njia sahihi ya kuwatumia wote Luis Suarez na Daniel Sturridge kikosini, bila kupunguza idadi ya viungo. Mfumo wa 3-4-1-2 umefanya vizuri dhidi ya Sunderland na Crystal Palace, lakini bado kupimwa dhidi ya timu kubwa.
Kuna watu wanadai kwamba mfumo huu ulitumiwa na Rodgers kutokana na kukosekana kwa Glen Johnson.
Tatizo la Liverpool ni ubutu wa viungo wake kwenye kufunga, Rodgers anatakiwa kusajili kiungo mfungaji Januari na kupunguza kuwategemea sana Suarez na Sturridge.
Tatizo lingine Liverpool ni kwamba hakuna watu sahihi wa kuziba nafasi za Lucas Leiva na Steve Gerrard. Jordan Henderson amekuwa na msimu mzuri, lakini Livepool bado wanahitaji mbadala wawili hawa. Joe Allen anaweza kucheza nafasi ya Gerrard, lakini bado hana roho ya mapambano.
Chelsea
Fowadi butu
Mastaa wengi
Baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Manchester United, Chelsea ilipoteana, lakini sasa imezinduka na kuanza kutoa dozi wana pointi mbili nyuma ya Arsenal.
Mastraika wa Chelsea ndiyo tatizo kubwa la Jose Mourinho, kwa sababu hawafungi. Ujio wa Samuel Eto’o haujabadilisha kitu, Fernando Torres na Demba Ba wameendelea kuwa butu mbele ya goli.
Eto’o aliletwa kumaliza tatizo la ufungaji, lakini Mcameroon bado hajazoea Ligi Kuu England. Mourinho anatakiwa kusajili straika Januari.
Tatizo lingine kwa Mourinho ni kukosa kombinesheni nzuri kwenye kiungo. Chelsea imejaza mastaa wengi kwenye eneo la kiungo na ni ngumu kuwafurahisha wote.
Kuwachezesha kwa kupokezana, kunaharibu kujiamini na kuzoeana kwa wachezaji na moto wa kikosi unapungua. Mourinho anahitaji kujua kikosi chake cha kwanza.
Manchester City
Ukuta mbovu
Tatizo la Fernandinho-Toure
Manchester City wameanza vibaya msimu huu. Manuel Pellegrini anahitaji muda kuzoea ligi na kuingiza falsafa yake Etihad.
Man City msimu huu wamekuwa wakifunga mabao watakavyo, mpaka sasa wana mabao 20 kwenye mechi nane. Hilo lilitarajiwa kutokana na ukubwa wa safu yao ya ushambuliaji.
Lakini tatizo kubwa la Man City ni nyuma, beki yao inapitika kirahisi, kukosekana kwa Vincent Kompany kunawatesa. Tatizo lingine liko golini kwa Joe Hart amekuwa akifungwa kizembe.
Kuondoka kwa Gareth Barry, kumewafanya Man City kumtumia Fernandinho na Yaya Toure katikati, hawa wote wawili ni wazuri sana, lakini wanacheza soka la kufanana na City wanahitaji kiungo wa kukaa na kulinda mabeki.
Tottenham Hotspur
Mabao yamekauka kwa Soldado
Matatizo kwenye winga
Roberto Soldado alisajili Spurs kuja kufunga mabao, lakini mpaka sasa hali imekuwa tofauti, ameshindwa kabisa kuongoza mashambulizi ya timu hiyo.
Spurs wanabeki bora England, lakini tatizo lao kubwa ni kushindwa kufunga mabao, mpaka sasa baada ya mechi nane wana mabao nane tu.
Kama Andre Villas Boas na jeshi lake wanataka kumaliza Top 4 au kuchukua ubingwa, wanatakiwa kuanza kufunga mabao kwenye mechi zao.
Roberto Soldado alisajiliwa kwa ajili ya kufunga, lakini Mhispaniola huyo bado hajafanikiwa kutimiza wajibu wake.
Pia Spurs inatatizo la kukosa winga hasa kutokana na kukosekana kwa Aaron Lennon. Andros Townsend na Gylfi Sigurdsson wanaofanya vizuri, lakini wanapenda kuingia ndani. Nacer Chadli na Erik Lamela siyo mawinga halisi nao.
Manchester United
Fellaini bado sana
Mawinga majanga
Manchester United wameanza msimu vibaya sana chini ya David Moyes. Mpaka sasa hivi wameshinda mechi tatu kati ya nane. United wana nafasi ya kufufuka.
Kikosi cha United kinakosa ubunifu na David Moyes bado hajajua namna ya kumtumia Shinji Kagawa, siku akijua namna ya kumtumia tatizo hilo litamalizika.
Man United wanamtegemea sana Wayne Rooney, mawinga wa timu hiyo wamekuwa doro sana, Ashley Young na Antonio Valencia wamechemsha, wakati Luis Nani hajapata nafasi ya kutosha. Adnan Januzaj (18) anajua, lakini ni mapema mno kuanza kumtegemea.
Ujio wa Marouane Fellaini ulitarajiwa kumaliza tatizo kwenye kiungo cha United, lakini United bado inamtegemea Michael Carrick (32), David Moyes anaweza kulazimika kusajili kiungo mwingine Januari.
Rio Ferdinand anaelekea kumaliza, wakati Phil Jones na Chris Smalling bado hawajaonyesha ubora wao. Ferdinand anadai kwamba anahitaji kupumzika. Moyes anatakiwa kutafuta msaidizi mzuri wa Rafael kulia, kwa sababu Jones na Smalling wamechemsha idara hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment