Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, September 30, 2013

SIMBA YAZIDI KUJIIMARISHA KILELENI YAICHAPA JKT RUVU 2-0






SIMBA imeendelea kuchanja mbuga baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa jana, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba imezidi kuwaacha watani wao wa jadi Yanga kwa tofauti ya pointi tano, huku ikiendelea kukaa kileleni kutokana na pointi 14, huku ikiwa haijafungwa zaidi ya kutoka sare mechi mbili na kushinda  mechi nne. 

JKT Ruvu iliyoanza ikiongoza katika msimamo wa ligi hiyo kabla ya Simba, imeshuka hadi nafasi ya saba  kutokana na pointi tisa sawa na Yanga inayoshika nafasi ya tano huku Azam FC ikipanda hadi nafasi ya nne kutokana na sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons jana na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 10 sawa na Coastal Union inayoshika nafasi ya tatu huku Kagera Sugar inaifuatia Simba, baada ya kujikusanyia pointi 11 na Ruvu Shooting ikiwa nafasi ya sita kutokana na pointi tisa, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi sita kila moja.

Katika mechi ya jana, Simba ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la JKT Ruvu ikiwa ni dakika ya saba, baada ya Amis Tambwe kupiga shuti kali akitumia krosi ya Amri Kiemba, lakini alitokea Shaban Dihile na kuokoa hatari hiyo.

Dakika ya 17, Abdulhalim Humud alioneshwa kadi ya njano kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji wa JKT Ruvu, Salum Machaku.
Hata hivyo, JKT Ruvu ilipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 21, baada ya beki wa timu hiyo, Stanley Nkomola kupiga krosi iliyomkuta Damas Makwaya na kupiga shuti ambalo liliokolewa na Kipa wa Simba, Abel Dhaira.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na Mwamuzi, Antony Kayombo kutoka Rukwa, alitoa penalti kwa Simba dakika ya 24, iliyoonwa na mwamuzi wa pembeni, John Kanyenye, baada ya beki wa JKT Ruvu, Jamal Said kunawa mpira katika eneo la hatari iliyofungwa na Tambwe na kumfanya akifikishe mabao saba.
Katika dakika ya 43, Makwaya aliwatoka mabeki wa Simba na kuachia shuti kali, lakini kutokana na ushupavu wa Kipa, Abel  Dhaira aliondoa hatari hiyo.

Simba ilipata bao la pili kupitia kwa Ramadhan Singano ‘Messi’ aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kiemba, aliyefunga bao la moja kwa moja baada ya kuunganisha krosi ya Humud.
JKT Ruvu walipoteza nafasi ya kufunga baada ya Emmanuel Pius kupiga shuti kali katika dakika ya 80, lakini Kipa wa Simba, Dhaira aliweza kupangua shuti hilo.

Simba iliwakilishwa na wachezaji, Abel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoun Seif, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Amri Kiemba, Said Ndemla, Amis Tambwe, Betram Mombeki, na Haruna Chanongo.

JKT Ruvu: Shaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omari Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftal, Alhaji Zege, Emmanuel Swita/ Richard Msenya (dk 58), Bakari Kondo/Paul Ndauka (dk 78), Salum Mchaku na Emmanuel Pius.

Wakati huo huo, Azam FC imetoka sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Bao la Tanzania  Prisons lilifungwa na Peter Michael katika dakika ya 36 na, lilifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 49.

Katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Ashanti United imetoka sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment