Golikipa wa Mgambo JKT, Kulwa Manzi akiwa chini baada ya
kupishana na mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe (kulia)
wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda 6-0.
Washambuliaji wa simba, Amisi Tambwe (kulia), na Betram Mombeki wakishangilia ushindi wa timu yao.
Haruna Chanongo akimtoka kiungo wa timu ya Mgambo JKT, Salum kipaga.
Mashabiki wa Simba.
Amri Kiemba akiwatoka wachezaji wa Mgambo JKT.
Hakuna njia hapa.
Beki wa Mgambo JKT, Bakari Mtama akimiliki m[pira huku akizongwa na mshambuliaji wa simba, amis Tambwe.
Betram Mombeki akiwatoka mabeki wa Mgambo JKT.
Wachezaji wa Simba.
Wakifuatilia pambano hilo.
Waamuzi wa mchezo huo.
SIMBA raha bwana!
Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 katika mechi
ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, huku Yanga ikibanwa na Tanzania Prisons baada ya kutoka sare ya bao
1-1, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Kwa ushindi huo, Simba
imeweza kufikisha pointi 10 ikiiengua kileleni JKT Ruvu iliyokuwa ikiongoza kwa
pointi tisa ambayo jana ilifungwa na Ruvu Shooting, katika mechi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Simba imefikisha
pointi hizo, baada ya kushinda mfululizo mechi tatu dhidi ya JKT Oljoro bao
1-0, kisha mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo ilitoka sare ya mabao 2-2 na
Rhino Rangers.
Mechi hiyo
iliyochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo, Simba waliandika bao la kwanza katika dakika ya nne lililofungwa na
mshambuliaji wa kimataifa kutoka Burundi, Amisi Tambwe kwa kichwa, baada ya
kuunganisha krosi ya beki wa pembeni, Issa Rashid.
Simba ilikosa bao
katika dakika ya saba, baada ya Henry Joseph kushindwa kutumia pasi nzuri ya
Batrem Mombeki aliyepiga shuti hafifu lililodakwa na Kipa wa Mgambo Shooting,
Kulwa Manzi.
Katika dakika ya 12, Simba ilipoteza nafasi
nyingine ya kufunga, baada ya Tambwe kupiga shuti kali ambalo liliwachanganya
mabeki wa Mgambo, lakini kipa Manzi aliwahi na kuokoa hatari hiyo.
Mgambo Shooting
walifanikiwa kufanya shambulizi zuri dakika ya 20, ambapo Salum Kipaga aliachia
shuti kali, lakini alishindwa kufunga ambalo lilitoka sentimeta chache kutoka
lango la Simba.
Dakika ya 30, Mombeki
alishindwa kuipatia Simba bao la pili, baada ya kupiga shuti kali ambalo
lilitoka nje kidogo ya lango la Mgambo Shooting, ambaye alimalizia kazi nzuri
iliyofanywa na Rashid.
Simba walipata bao la
pili katika dakika ya 32 kupitia kwa Haruna Chanongo baada ya kuwachambua
mabeki wa Mgambo Shooting na kufanikiwa kumpiga kanzu Kipa, Kulwa Manzi na
mpira kujaa vyavuni.
Tambwe alifunga bao la tatu katika dakika ya 41,
baada ya kipa wa Mgambo Shooting, Manzi
kutema shuti la Chanongo na kumkuta mfungaji, ambapo Tambwe alifunga tena
dakika ya 44 akimalizia pasi ya mwisho ya Amri Kiemba.
Hata hivyo, kipa wa Mgambo alifanya kazi ya
ziada kuokoa krosi iliyopigwa na Tambwe
ambapo Mombeki alikuwa anaisubiria kwa hamu ili aweze kupachika bao.
Mwamuzi, Adongo
alimwonesha kadi ya njano beki wa Simba, Adam Miraji dakika ya 49 baada ya
kumchezea rafu winga wa Mgambo Shooting Salum Gila.
Simba ilipata bao la
tano, dakika ya 61, baada ya beki wa Mgambo Shooting, Bakari Mtama kujifunga
mwenyewe akiwa katika harakati ya kuokoa krosi iliyochongwa na Chanongo
.
Dakika ya 77, Tambwe
alifunga bao la sita kwa Simba kwa njia ya penalti, baada ya Salum Kipanga
kuunawa mpira eneo la hatari na Mwamuzi wa mechi hiyo, Adongo kuamuru ilipigwe
penalti hiyo.
Baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo,
alisema matokeo yanatokana na mbinu ambazo amekuwa akiwafundisha wachezaji na
anatarajia wataendelea kushinda mechi inayofuata dhidi ya Mbeya City
itakayochezwa Jumamosi kwenye uwanja huo.
Kwa upande wa Kocha wa Mgambo Shooting, Mohamed
Kampira alimtupia lawama kipa wake, Kulwa Manzi kwa kuruhusu mabao ya kizembe
aliyofungwa katika mechi hiyo.
Simba iliwakilishjwa na: Abel Dhaira, Adam Miraji, Issa Rashid, Kaze
Gilbert, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Amisi Tambwe, Henry
Joseph, Batrem Mombeki na Haruna
Chanongo.
Mgambo Shooting iliwakilishwa na: Kulwa Manzi, Francis Anyosisye, Salum Mlima,
Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga,
Nassor Gumbo, Peter Mwalianzi, Mohamed Neto, Fully Maganga na Salum Gila.
YANGA imebanwa tena baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons,
katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya.
Yanga ilikuwa ya
kwanza kulifikia lango la Tanzania Prisons, ambapo Didier Kavumbagu alikosa bao
katika dakika ya tatu baada ya kuwatoka mabeki wa Prisons na kupiga shuti kali ambalo lilitoka nje.
Mechi hiyo
iliyochezeshwa na Simon Mbelwa kutoka Pwani, Prisons ilikosa bao katika dakika
ya 19, baada ya Six Ally kushindwa kumalizia krosi ya Laurian Shaban, lakini
Kipa wa Yanga, Ally Mustapha aliondoa hatari hiyo.
Katika dakika ya 14,
Jeryson Tegete aliifunga Yanga bao la kuongoza baada ya kumalizia krosi ya
Simon Msuva kutoka winga ya kulia.
Dakika ya 59 beki wa
Prisons, Jimmy Shoji alifanya kazi ya ziada baada kuokoa shuti la Tegete,
lililoelekea kuzama langoni mwao.
Yanga ilipoteza nafasi
ya kufunga dakika ya 75, baada ya Kavumbagu kuunganisha kwa kichwa mpira
uliopigwa na beki wa pembeni wa timu hiyo, Mbuyu Twite, lakini Kipa wa Prisons
aliokoa hatari hiyo.
Prisons walisawazisha
katika dakika ya 76 kupitia kwa kiungo wa timu hiyo, Michael Petes, baada ya
kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Omega Seseme aliyetokea benchi kuchukua
nafasi ya Jermia Juma, aliyefunga kwa kichwa. Hata hivyo, Yanga ilipoteza
nafasi nyingine ya kufunga baada ya Said Bahanunzi kushindwa kumalizia krosi ya
Kavumbagu katika dakika ya 87 akiwa ndani ya eneo la 18.
Baada ya mechi hiyo,
mashabiki wa Yanga waliangua kilio kwa madai timu yao inahujumiwa baada ya wiki
iliyopita kutoka sare kama hiyo na Mbeya City iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Tanzania Prisons: Beni David, Salum Kimenya, Laurian Shaban,
Jumanne Elfadhili, Nurdin Issa, Jimmy Shoji/Hamis Rataon, Fredy Chucu, Ibrahim
Isaka, Six Ally, Jermia Juma/Omega Seme na Lugano Mwagomba.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan,
Salum Telela/Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Jeryson Tegete/Said Bahanuzi na
Haruna Niyonzima.
Uwsanja wa Chamazi, Azam
FC jana iling’ang’aniwa na Ashanti United, baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Mabao ya Azam FC
yalifungwa na Kipre Tchetche katika dakika ya 21, ambapo Mwamuzi wa mechi hiyo,
Oden Mbaga alimwonesha kadi nyekundu, Aggrey Morris dakika ya 60 kutokana na
kumchezea faulo, Hussein Sued. Bao la Ashanti United lilifungwa na Anton
Matangalu katika dakika ya 79 lililotokana na mpira wa adhabu ndogo.
MTIBWA Sugar imetoshana
nguvu sawa na Mbeya City, baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Huko Kagera timu ya
Kagera Sugar, imeonja ushindi baada ya kuifunga JKT Oljoro mabao 2-1 katika
mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mabao la Kagera Sugar
yalifungwa na Godfrey Wambura dakika ya 25 na Maregesi Mwangwa dakika ya 90,
huku bao la JKT Oljoro likifungwa na Shaibu Nayopa dakika ya 35.
Huko Tanga, Coastal
Union imeshindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani wa Mkwakwani, Tanga, baada ya
kutoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers.
Bao la kuongoza la
Rhino Rangers lilifungwa na Salum Majid katika dakika ya 26, baada ya kutokea
piga nikupige langoni mwa Coastal Union.
Bao la Coastal Union,
lilisawazishwa na Jery Santo kwa njia ya penalti katika dakika ya 81
iliyotolewa na Mwamuzi, Jacob Zakaria kutoka Pwani, baada ya Saada Kipanga
kunawa mpira eneo la hatari.
Nayo RUVU Shooting imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, katika
mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Bao la Ruvu Shooting,
lilifungwa na Stephano Mwasyika dakika ya 37 baada ya kupokea pasi kutoka kwa
Cosmas Lewis.
No comments:
Post a Comment