KLABU ya Chelsea
imethibitisha kwamba imeamua kumpeleka kwa mkopo straika wake aliyekosa penati
katika mechi ya Super Cup dhidi ya Bayern Munich, Romelu Lukaku, kwenye kikosi
cha Everton kwa msimu mzima.
Mtandao wa
Goal.com ulibaini juzi usiku kuwa straika huyo mwenye umri wa miaka 20, raia wa
Ubelgiji, amekubali kutua ndani ya dimba la Goodison Park, na alikuwa
Merseyside hadi juzi usiku, muda mchache kabla ya kufungwa kwa dirisha la
usajili, kwa ajili ya kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Lukaku amekwenda
kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya kikosi cha Roberto Martinez,
baada ya kiungo mshambuliaji wa timu, Marouane Fellaini, kutimkia Manchester
United na Victor Anichebe kwenda West Brom.
"Romelu
Lukaku ataendelea na msimu wa pili wa Ligi Kuu ya England akiwa nje kwa mkopo
na safari hii atatimkia kwenye kikosi cha Everton," Chelsea ilitoa taarifa
kupitia mtandao wake juzi.
"Kupelekwa
kwake Goodison Park kunafuatia mafanikio mazuri aliyoyapata msimu uliopita,
alipokuwa kwenye kikosi cha West Bromwich Albion ambako alicheza mechi 38 na
kufunga mabao 17, na kuwa mfungaji bora zaidi mwenye umri mdogo kwenye Ligi Kuu
ya England tangu Michael Owen alipofanya hivyo msimu wa 1998/99."
Lukaku mwenyewe
alithibitisha mapema kupitia mtandao wake wa Twitter akisema: "Nimesaini
Everton kwa mkopo wa msimu mpya."
No comments:
Post a Comment